1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Kikosi cha Kiafrika kuilinda serikali Somalia

7 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CClw

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kwa kauli moja hapo jana kuidhinisha kikosi cha kulinda amani cha kanda kuilinda serikali dhaifu ya Somali ambayo iko chini ya shinikizo linaloongezeka kutoka kwa wanamgambo wa Kiislam na pia imeruhusu kuodolewa kwa kiasi fulani vikwazo vya silaha dhidi ya nchi hiyo ili kuwezesha kupatiwa silaha kwa kikosi hicho cha Kiafrika.

Azimio hilo lililodhaminiwa na Marekani limewataka wanamgambo wa Kiislam waliodhibiti mji mkuu wa Somalia Mogadishu na karibu eneo lote la kusini mwa Somalia tokea mwezi wa Juni kukomesha kuendelea zaidi kujitanuwa kijeshi na kujiunga na serikali ya mpito katika mazungumzo ya kufanikisha suluhisho la kisiasa kwa amani katika nchi ambayo haikuwa na serikali inayofanya kazi tokea mwaka 1991.

Azimio hilo limetishia kuchukuliwa hatua na Baraza la Usalama dhidi ya wale wanaokwamisha juhudi za amani au kujaribu kuipinduwa serikali.

Na wakati ikiruhusu kikosi cha Afrika kutumia silaha kuihami serikali Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa limetishia kuweka vikwazo kwa wengine wanaokiuka vikwazo vya silaha dhidi ya Somalia vilivyowekwa hapo mwaka 1992 kutokana na mapigano miongoni mwa wababe wa vita baada ya kumpinduwa dikteta Siad Barre.