Ndege za Kenya zashambulia ngome ya Al Shababu na kuua 14 | Matukio ya Afrika | DW | 16.01.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Ndege za Kenya zashambulia ngome ya Al Shababu na kuua 14

Jeshi la Kenya limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya kambi ya wanamgambo wa al Shabab nchini Somalia na kuua wanamgambo saba.

Jeshi la Kenya liliingia nchini Somalia mwishoni mwa mwaka jana kupambana na Al Shababu

Jeshi la Kenya liliingia nchini Somalia mwishoni mwa mwaka jana kupambana na Al Shababu

Mashambulizi hayo yalilenga kambi ya al Shabab katika mji wa Jilib ulioko umbali wa kilomita 120 kutoka mji wa bandari wa Kismayu yaliko makao makuu ya wanamgambo hao.

Wanamgambo wa Al Shababu na wananchi wa kawaida katika mji wa Jilib wamethibitisha kufanyika kwa mashambulizi hayo na kuongeza kwamba mbali na wapiganaji saba waliouawa, familia ya watu saba pia iliangamizwa katika mashambulizi hayo. Kiongozi wa kiukoo, Abdullahi Wayo Arag ameliambia shirika la Habari la Reuters kuwa familia hiyo lilikuwa pamoja kwenye chakula cha mchana nyumba yao ilipopigwa na bomu.

An Ethiopian soldier radios headquarters upon the arrival in the port city of Kismayu after dislodging Islamic fighters from their last remaining stronghold in Somalia on Monday 1 January 2007. Government forces backed by Ethiopian troops took control Somalia's third largest city when soldiers from the Islamic Courts Union abandoned their positions after a night of heavy shelling and advanced with tanks, aircraft and a large contingent of troops. Witnesses report seeing hundreds of Islamic fighters many of them Arabs and South Asians fleeing the town in the direction of neighboring Kenya. Ethiopian troops officially entered Somalia on 24 December, joining fighters loyal to Somalia's interim government, to repel an Islamist assault on the government stronghold of Baidoa. EPA/IBRAHIM ELMI +++(c) dpa - Report+++

Wanamgambo wa Al Shababu wamekuwa wakihama maeneo yanayotekwa na jeshi la Kenya

Msemaji wa serikali ya mpito wa Somalia Mahmoud Farah pia alikubali kwamba kambi mbili za Al Shababu zilishambuliwa na jeshi la Kenya ambao ni washirika wa serikali ya mjini Mogadishu. Msemaji huyo pia alikiri kutokea kwa vifo vya raia.

Hakukuwa na taarifa zozote kutoka upande wa Kenya, ingawa jeshi la nchi hiyo lilitangaza mwishoni mwa juma kwamba lilikuwa likiukaribia mji wa Kismayu, na kwamba liko tayari kuuteka mji huo muda ukiwadia.

Jeshi la Kenya liliingia nchini Somalia baada ya mashambulizi kadhaa ya wanamgambo wa Al Shababu ndani ya Kenya, ambayo yalitishia kuvuruga sekta ya utalii na kuyumbisha kanda nzima. Nchi nyingine jirani, Ethiopia iliingia tena kijeshi ndani ya Somalia majuma mawili yaliyopita, kuiunga mkono serikali ya nchi hiyo ambayo inalindwa na vikosi vya umoja wa Afrika.

Wakati hayo yakitokea, polisi ya Kenya ilitangaza jana kukamatwa kwa kundi la raia 29 wa Uganda ambao walituhumiwa kuwa safarini kwenda Somalia kujiunga na wanamgambo wa Al Shababu. Kundi hilo la wanaume 27 na wanawake 2 lilikamatwa mjini Nairobi baada ya polisi kudokezewa na wakaazi ambao walishuku mienendo yao.

Uwezo wa wanamgambo wa Al Shababu kusajili wapiganaji wapya kutoka nchi jirani, hasa Kenya, Tanzania na Uganda umekuwa ukivitia wasi wasi vyombo vya usalama vya kikanda. Mwezi Julai mwaka jana Umoja wa Mataifa ulitahadharisha kwamba Al Shababu ilikuwa ikiandikisha wapiganaji wapya, kuchangisha fedha na hata kuendesha mafunzo ndani ya Kenya. Tahadhari hiyo ya Umoja wa mataifa ilibainisha kuwa wengi wa vijana wanaojiunga na kundi hilo ni wale walioingia dini ya kiislamu hivi karibuni, na wengine ambao wanahadaiwa kwa pesa.

Miongoni mwa washukiwa wa shambulizi la kigaidi lililoua watu 76 mjini Kampala Julai mwaka 2010, kuna raia wengi wa Kenya. Hivi karibuni, kundi lenye msimamo mkali wa kiislamu nchini Kenya, Muslim Youth Center limetangaza kuwa mkuu wake ameteuliwa kuwa mwakilishi wa Al Shababu, hatua ambayo bila shaka itazidisha wasi wasi juu ya hali inayoikabili Kenya ndani Somalia. Kundi hilo, Muslim Youth Center, lilitajwa katika ripoti ya umoja wa mataifa ya mwaka jana, kama mojawapo ya wasaidizi wa Al Shababu.

Hata hivyo nguvu za Al Shababu zimekuwa zikipungua katika siku za hivi karibuni, baada ya kuandamwa na vita kutoka pande mbali mbali, zikiwemo Kenya upande wa Kusini, Ethiopia upande wa magharibi, na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na umoja wa Afrika kutokea upande wa kaskazini.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/AP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu