1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchini Iraq umwagikaji wa damu ungali unashuhudiwa.

10 Aprili 2007

Hii leo kiasi watu 42 wameuwawa na wengi kujeruhiwa katika mashambulio yaliyofanyika katika maeneo mbali mbali ya mji wa Baghdad

https://p.dw.com/p/CHGb

Wairaqi kiasi 16 wameuwawa na wengine 30 wakajeruhiwa hii leo baada ya mwanamke kujitoa muhanga kwa kujiripua nje ya kituo cha kujiandikisha kujiunga na polisi huko kaskazini mashariki mwa mji wa Baghdad.Shambulio hilo limetajwa kuwa baya zaidi kuwahi kufanyika dhidi ya wanaojitolea kujiunga na vikosi vya usalama nchini iraq mwaka huu.

Kwa mujibu wa walinzi wa kituo hicho pamoja na maafisa wa polisi shambulio hilo limefanywa na mwanamke aliyevalia buibui na kujifunga mkanda alioujaza miripuko.

Mashahidi wanasema mwanamke huyo aliyekuwa amejitia miongoni mwa makuruta alijiripua mbele ya mlolongo wa makuruta hao waliokuwa wamepanga foleni ya kupeleka stakabadhi zao za kujiandikisha kujiunga na polisi.

Kwengineko watu sita wameuwawa na wengine 20 kujeruhiwa katika shambulio la bomu lililotegwa kandokando ya barabara kwenye eneo lenye shughuli nyingi la al-Gadiriyah kusini mwa Baghdad.

Wakati hayo yakiarifiwa katika eneo la kati mwa Baghdad kumeripotiwa mapigano makali kati ya wanajeshi wa Marekani na vikosi vya Iraq dhidi ya wapiganaji katika wilaya ya Fadhil ambako ni ngome ya waasi wakisunni.

Opresheni hiyo kali kabisa inalenga maficho ya waasi na makundi ya wanamgambo wenye sialaha wanaofikiriwa kuhusika na machafuko mjini Baghdad.

Wairaqi kiasi 20 wamuwawa wakiwemo watoto na wanawake na watu wengine 30 wamejeruhiwa kwenye mapambano hayo.

Wakaazi wa eneo hilo wamedai kwamba Helikopta za wanajeshi wa Marekani zinavurumisha risasi katika maeneo yaliyo na shughuli nyingi za kibiashara huku vikosi vya nchi kavu vikirusha gesi za kutoa machozi.

Wanajeshi wa Marekani wamefahamisha kwamba kuna opresheni inayoendelea katika eneo hilo na kwamba ndege yao ya Helikopta aina ya Apache imeshambuliwa kwa silaha ndogo ndogo katika eneo hilo na hivyo ilibidi kurudi kambini.

Hapo jana wanajeshi wanne wa Marekani waliuwawa na kuufanya mwezi wa April kuelekea kuwa mwezi mbaya zaidi wa mashambulio dhidi ya vikosi vya Marekani mwaka huu.

Wanajeshi 45 wa Marekani wameuwawa nchini Iraq mwezi huu pekee nusu yao wameuwawa katika mji wa Baghdad.

Rais Gorge Bush lakini anapeleka kikosi zaidi cha wanajeshi 30 elfu nchini Iraq kuoengeza nguvu mapambano dhidi ya waasi mjini Baghdad.

Hatua hii ya Bush inaonekana na wengi kama ndio nafasi ya mwisho kabisa ya kujaribu kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iraq.

Licha ya kwamba wanajeshi wa Iraq wamepata mafunzo mapya kutoka kwa wanajeshi wa Marekani serikali ya waziri mkuu Nuri al Maliki bado lakini inategemea pakubwa silaha na usaidizi wa kijeshi kutoka Kwa Marekani.

Kwa upande mwingine rais Bush amekataa kuweka ratiba ya kuondoa wanajeshi wake na amesisitiza kwamba wanajeshi wa Marekani hawataondoka Iraq hadi pale wairaqi watakapomudu usalama wa nchi yao.