1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi kubwa zaujadili mswada kuhusu Syria

18 Septemba 2013

Wanadiplomasia kutoka nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanakutana mjini New York kujadili mswada wa azimio linalohusu kuteketezwa kwa silaha za sumu za Syria.

https://p.dw.com/p/19jrt
Wataalamu wa silaha wa Umoja wa Mataifa wakiwa kazini nchini Syria
Wataalamu wa silaha wa Umoja wa Mataifa wakiwa kazini nchini SyriaPicha: Reuters

Majadiliano hayo yanawashirikisha wanadiplomasia kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China, ambao wanauangalia mswada huo kabla ya kuufikisha mbele ya baraza zima lenye nchi 15 wanachama. Mswada huo unalenga kuunga mkono makubaliano yaliyopatikana kati ya Urusi na Marekani mjini Geneva Jumamosi iliyopita, ambapo Syria ilitakiwa kutoa maelezo kamili juu ya silaha zake za sumu na kutoa ushirikiano katika kuzitekeza.

Wanadiplomasia katika Umoja wa Mataifa wamesema bado haijulikani lini kura itapigwa juu ya mswada huo, ambao unaacha mlango wazi kwa matumizi ya nguvu ikiwa Syria itashindwa kuutekeleza ipasavyo. Washiriki kutoka Urusi wanataka kipengele hicho cha matumizi ya nguvu kiondolewe.

Katibu Mkuu ahimiza juu ya muafaka

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelitolea wito Baraza la Usalama na hususan Marekani na Urusi kupata muafaka ili majadiliano hayo yaweze kupiga hatua.

Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaPicha: Reuters

''Ni matumaini yangu ya dhati kwamba Urusi na Marekani zitadhihirisha sifa zao za uongozi kwa wakati huu, na pia wanachama wengine wa kudumu wa baraza la usalama, hawana budi kutambua na kutekeleza majukumu yao muhimu ya kihistoria na kisiasa.'' Amesema Ban.

Wito mwingine kama huo wa katibu mkuu Ban Ki-moon umetolewa na mfalme wa Jordan Abdullah, ambaye ameitaka China kutumia nafasi yake kama mwanachama wa kudumu katika baraza la usalama kutoa mchango zaidi katika kusuluhisha mzozo wa Syria.

Mfalme Abdullah ameyasema hayo wakati alipokutana na rais wa China Xi Jinping mjini Beijing. Hadi waandishi wa habari walipoondolewa kwenye ukumbi wa mkutano, rais Xi alikuwa hajatoa jibu kwa rai hiyo.

Obama asema sharti Assad aondoke

Wakati huo huo, rais wa Marekani Barack Obama ambaye siku za nyuma alitishia kuishambulia kijeshi Syria amesema hata baada ya kuteketezwa silaha za sumu za nchi hiyo, rais Bashar al-Assad atalazimika kuondoka ili kutoa nafasi kwa kipindi cha mpito.

Bashar al-Assad, rais wa Syria anaekabiliwa na shinikizo
Bashar al-Assad, rais wa Syria anaekabiliwa na shinikizoPicha: imago/UPI Photo

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Uhispania, Telemundo, rais Obama amesema ni vigumu kufikiria kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, wakati rais Bashar al-Assad akibakia madarakani. Amesema mchakato huo utakwenda hatua kwa hatua, na kuongeza kwamba hatua inayopigwa kwa wakati huu ni kuondoa silaha za sumu.

Na katika uwanja wa mapambano nchini Syria, bomu la kutegwa ndani ya gari limeripuka kwenye kivuko cha Bab al-Hawa kwenye mpaka kati ya Syria na Uturuki, unaodhibitiwa na waasi. Shirika linalochunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao mjini London limesema kuwa watu 12 wamejeruhiwa katika mripuko huo. Hakuna taarifa zozote kuhusu aliyefanya shambulizi hilo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AP/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman