1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Nawaz Sharif kurejea Pakistan

Mahkama kuu ya pakistan imetoa hukumu kwamba waziri mkuu wa zamani wa Pakistan,Nawaz Sharif ni ruhusa kurejea nyumbani. Sharif alitimuliwa madarakani 2000 na jamadari Musharaf na kwenda uhamishoni saudi Arabia.

Magazeti ya Pakistan yamekaribisha leo hukumu ya Mahkama Kuu kuwa waziri-mkuu wa zamani Nawaz Sharif anaeishi uhamishoni mjini London,Uingereza, anaweza sasa kurejea nyumbani.

Magazeti hayo yanasema kuwa,hukumu hiyo itakua na athari kubwa za kisiasa kwa jamadari Musharraf katika mwaka huu wa uchaguzi nchini Pakistan.

Nawaz Sharif,mara mbili waziri mkuu wa Pakistan,amekuwa akiishi uhamishoni nje ya Pakistan tangu mwaka 2000.Mwaka uliotangulia,mkuu wa majeshi,jamadari Pervez Musharraf alimuangusha madarakani katika mapinduzi yasiomwaya damu na yaliokaribishwa mikono miwili na wapkistani wengi nchini.

Kufuatia uamuzi wa Mahkama Kuu ya Pakistan kuwa aweza sasa kurejea nyumbani,Nawaz Sharif aliwaambia maripota jana mjini London kuwa atarudi Pakistan, tena karibuni ili kugombea uchaguzi ujao.

Kurejea kwake nchini yamkini kukatatanisha juhudi za rais Musharraf kujipatia kipindi kingine cha kuitawala Pakistan-nchi yenye silaha za kiunuklia ambayo ni ufunguo kwa sera za Marekani za kupambana na ugaidi na kuituliza Afghanistan.

Nawaz Sharif baada ya hukumu ya jana alisema:

“Tunabidi kulirejesha jeshi kambini nah ii yafaa kuwekwa wazi kabisa.Pia inabidi pawepo utawala wa kisheria nchini Pakistan na katiba lazima iheshimiwe.”

Wakati hukumu ya mahkama inaimarisha matumaini ya Nawaz Sharif na chama chake cha Pakistan Muslim League-hukumu hiyo yaweza pia kumuathiri waziri mkuu mwengine wa zamani aishie uhamishoni,bibi Benazir Bhutto.Bhutto amekuwa akijadiliana faraghani kugawana madaraka na jamadari Musharraf.”Hukumu hii imemuweka Benazir Bhutto na chama chake cha Pakistan Peoples Party katika hali mbaya.”-gazeti moja la Pakistan –THE DAWN limeandika.

Nawaz Sharif aliejiambatisha upande mmoja na vyama vya kiislamu,amekuwa akiweka wazi wazi kwamba hana mpango wa kuridhiana na lolote lile na rais Musharraf.

Musharraf bado hakutamka lolote juu ya hukumu ya Mahkama ambayo ni pigo la pili kwake baada ya kurejeshwa madarakani hakimu mkuu aliesimamishwa kazi na Musharraf .

Msimamo huo lakini huweza ukamshawishi jamadari Musharraf kuitoa kabatini ile silaha yake aliotaka kuitumia karibuni ya kutangaza hali ya hatari.

Nawaz Sharif akifafanua zaidi nini anataka sasa

“Vyombo vya habari lazima view huru na hatutarudi nyuma juu ya masharti haya.”

Kusema kweli lakini, magazeti nchini Pakistan yamejionea uhuru mkubwa zaidi wa kuandika chini ya jamadari Musharraf anaetwala sasa kuliko chini ya waziri mkuu huyo wa zamani Nawaz Sharif.

Hukumu ya jana pia imemfungulia mlango ndugu wa Nawaz,Shhbaz -kiongozi mashuhuri wa Muslim League kurejea nyumbani.

Nawaz Sharif,alihamia Saudi Arabia baada ya kutimuliwa madarakani mwaka 2000 na utawala wa Musharraf kudai ameridhia kubakia nje kwa kipindi cha miaka 10.Binafsi,Sharif anakanushia kuridhia jambo hilo.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com