1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nawaz Sharif arejeshwa uhamishoni Saudi Arabia.

Sekione Kitojo10 Septemba 2007

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Nawaz Sharif amerejeshwa nchini Saudi Arabia leo Jumatatu , kiasi cha saa nne baada ya kuwasili nchini humo katika uwanja wa ndege wa mjini Islamabad akitokea nchini Saudi Arabia baada ya miaka kadha ya kuishi uhamishoni.

https://p.dw.com/p/CB1R

Vituo kadha vya televisheni nchini Pakistan vimeripoti kuwa Nawaz Shariff anarejeshwa nchini Saudi Arabia. Baadhi ya vyombo hivyo vya habari vimeripoti kuwa amesafirishwa kupitia shirika la ndege la kimataifa la Pakistan , baada ya vituo hivyo kuonyesha ndege hiyo ikiondoka kutoka uwanja huo wa ndege.

Nawaz Sharif aliishi uhamishoni kwa muda wa miaka saba baada ya kuangushwa kutoka madarakani na rais wa sasa wa Pakistan Pervez Musharaff miaka minane iliyopita.

Polisi walimtia mbaroni kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 57 kwa madai ya ulaji rushwa mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Islamabad kufuatia mvutano mkubwa kuhusiana na hati yake ya kusafiria. Aliondolewa nchini humo mara baada ya hapo, akitiwa katika ndege iliyokuwa ikiondoka kuelekea Saudi Arabia.

Sharif aliahidi kwamba kurejea kwake kutatoa msukumo wa mwisho katika udikteta wa Musharaff ambao unaporomoka, ambapo mkuu huyo wa jeshi na mshirika mkubwa wa Marekani , amekuwa taratibu akiona nguvu zake madarakani katika nchi hiyo zikidhoofika baada ya miezi kadha ya watu kuingia mitaani wakifanya maandamano.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kurejea kwa kiongozi huyo wa zamani aliyeondolewa madarakani katika mapinduzi ambayo hayakumwaga damu mwaka 1999 ingekuwa changamoto kubwa kwa Musharaff, ambaye anawania kubaki madarakani katika taifa hilo ambalo limeingia katika mtafaruku wa kisiasa.

Lakini serikali ya Musharaff , ambayo imekuwa ikishuhudia kuporomoka kwa umaarufu wake wakati mizozo inazidi nchini humo , haraka ilimrejesha Sharif nchini Saudi Arabia , nchi ambako alikuwa akiishi uhamishoni tangu mwaka 2000.

Wakati akirejea nchini Pakistan Nawaz Sharif aliwaambia waandishi wa habari kuwa anarejea nchini humo ili kubadilisha mambo ambayo amedai yalikuwa yanakwenda kombo.

Polisi ambao walikuwa wameshika virungu walipambana na kiasi cha watu 100 ambao wanamuunga mkono Sharif , na kuwakamata baadhi ya wanachama muhimu katika chama chake, wakati majeshi ya usalama yakiweka ulinzi mkali katika eneo la kilometa tano kuzunguka uwanja huo wa ndege wa Islamabad. Alisalimiana na watu wanaomuunga mkono ndani ya ndege mara ilipotua. Chama cha Sharif cha Pakistan Muslim League kimesema kuwa kimepeleka mashtaka katika mahakama kuu , kikisema kuwa mahakama iliiamuru serikali kutomzuwia kuingia nchini humo.