1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yajadili mkakati mpya wa usalama

Mohamed Dahman18 Novemba 2010

Viongozi wa nchi za Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO) wanakutana mjini Lisbon, Ureno, kuzungumzia mikakati mipya ya ulinzi na usalama kwenye eneo lao

https://p.dw.com/p/QCy6
Afisa wa Usalama akilinda eneo utakapofanyika mkutano wa NATO mjini Lisbon
Afisa wa Usalama akilinda eneo utakapofanyika mkutano wa NATO mjini LisbonPicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Ureno imechukua hatua kubwa za kuimarisha usalama kuwahi kushuhudiwa nchini humo kabla ya kuanza kwa mkutano wa Kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO mjini Lisbon hapo kesho kuepuka vurugu zilizochafua mkutano kama huo uliofanyika nchini Ufaransa hapo mwaka 2009 kuadhimisha miaka 60 ya jumuiya hiyo ambapo waandamanaji walipambana na polisi na kushambulia hoteli.

Tokea Jumanne polisi na helikopta zimekuwa zikipiga doria katika mipaka ya Ureno kuzuia makundi ya watu wenye siasa kali kufanya vurugu.

Katika mji mkuu wa Lisbon zimechukuliwa hatua kali za kuimarisha usalama tokea Jumatatu katika eneo lilioko nje ya mji huo ambapo viongozi wa nchi 60 na mashirika watakutana kwa siku mbili kuanzia kesho.Takriban wajumbe na waandishi wa habari 5,000 wanatazamiwa kuhudhuria.

Maafisa usalama 7,000 watakuwa kazini baina ya eneo la mkutano na katika mji mkuu wenyewe ambapo maandamano dhidi ya NATO yamepangwa kufanyika hapo Jumamosi.

Maandamano hayo makuu yameandaliwa na vyama vinavyopinga vita,vyama vya wafanya kazi na Chama cha Kikomunisti cha Ureno. Hata hivyo polisi ya Ureno imesema inaweza kudhibiti hali hiyo.

Rais Dmitry Medvedev wa Urusi atahudhuria mkutano huo wa viongozi wa NATO kuimarisha uhusiano na hasimu wake wa Vita Baridi wakati serikali ya Urusi bado ikionyesha mashaka juu ya mipango ya kuwa na makombora ya pamoja ya kujihami.

Medvedev atakuwa rais wa kwanza wa Urusi kuhudhuria mkutano wa viongozi wa NATO tokea kuzuka kwa mzozo wa vita vya nchi yake na Georgia hapo mwaka 2008 na Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen anaamini mkutano huo utakuwa fursa ya kupunga mashetani yaliopita.

Kuimarishwa kwa uhusiano wao kumekwamishwa na mipango ya mataifa ya magharibi ya kuweka makombora ya kujihami barani Ulaya zikiwemo nchi zilizokuwa kwenye kundi la kikomunisti hapo zamani ambayo Urusi inahofu kuwa yanawekwa dhidi yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle anasema suala la ushirikano wa usalama kati ya NATO na Urusi ni hatua kubwa.

Mkutano wa NATO unafanyika wakati Marekani ikiwa na wasi wasi mkubwa kwamba kupunguzwa kwa bajeti za ulinzi za Ulaya kunaweza kudhoofisha jumuiyo hiyo na kuiwacha Marekani bila ya kuwa na mshirika madhubuti wa kijeshi.

Mwandishi: Mohammed Dahman

Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhan