1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO, Urusi wakutana baada ya miaka miwili

20 Aprili 2016

Kwa mara ya kwanza baada ya kukunjiana nyuso kwa muda wa miaka miwili mabalozi wa mfungamano wa kijeshi wa NATO leo wanakutana na wajumbe wa Urusi kwenye baraza la pamoja.

https://p.dw.com/p/1IYs0
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Mabalozi wa NATO leo wanatarajiwa kukutana na wajumbe wa Urusi ili kuyaanzisha tena mazungumzo baina yao baada ya mvutano wa miaka miwili uliosababishwa na hatua ya Urusi ya kuliteka jimbo la Krimea la Ukraine na kuliweka chini ya udhibiti wake.

Stoltenberg ahimiza mdahalo

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kijeshi ya NATO Stoltenberg amesema ni muhimu sana kuendeleza mdahalo katika nyakati hizi za hatari na changamoto kubwa duniani. Bwana Stoltenberg hasa ametahadharisha juu ya hatari inayotokana na magaidi wa "Dola la Kiislamu".

Stoltenberg amesema kwenye baraza la pamoja la NATO na Urusi watajadili masuala ya uwazi katika shughuli za kijeshi na njia za kuepusha hatari.Ameeleza kuwa yaliyotukia kwenye bahari ya Baltik yanaonyesha umuhimu mkubwa wa kuwepo uwazi na kupunguza hatari.

Meli ya kijeshi kwenye bandari ya Wilhelm
Meli ya kijeshi kwenye bandari ya WilhelmPicha: picture-alliance/AP Photo/I. Wagner

Bwana Stoltenberg amesema wajumbe wa NATO na wa Urusi pia wataujadili mgogoro wa nchini Ukraine na njia zitakazochangia katika kujenga hali ya kuaminiana baina ya NATO na Urusi.

Uhusiano baina ya Ukraine na Urusi ulianza kutatizika baada ya kuondolewa madarakani kwa aliekuwa Rais wa nchi hiyo Viktor Yanukovich mnamo mwaka wa 2014. Urusi ilijibu kwa kuliteka jimbo la Ukraine -Krimea na kuliweka chini ya udhibiti wake.Urusi pia ilianza kuwaunga mkono waasi wa mashariki mwa Ukraine waliokuwa wanapigania kujitenga.

Kutokana na hatua hizo za Urusi ,jumuiya ya NATO ilisimamisha uhusiano wake na Urusi, kwa kueleza kuwa nchi hiyo ilivunja sheria ya kimataifa. NATO pia iliamua kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika nchi za Ulaya mashariki ambazo ni wanachama wa NATO.

Meli ya kijeshi kwenye bandari ya Wilhelm
Meli ya kijeshi kwenye bandari ya WilhelmPicha: picture-alliance/AP Photo/I. Wagner

Katika upande mwingine Urusi haikufurahishwa na hatua zilizochukuliwa na NATO katika nchi za Ulaya Mashariki.

Mazungumzo ya leo mjini Brussels baina ya mabalozi wa NATO na wajumbe wa Urusi hayatakuwa rahisi. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank - Walter Steinmeier ametahadharisha juu ya kuweka matumaini makubwa kuhusu mazungumzo hayo.

Na msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov amesema baada ya kuwindana katika miaka miwili iliyopita itakuwa changamoto kubwa kurejesha hali ya kuaminiana. Hata hivyo NATO imesema inadhamiria kuepusha mgongano na Urusi.

Mwandishi:Mtullya abdu.

Mhariri:Hamidou Oummilkheir