1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Nato kukabidhi jukumu la ulinzi Afghanstan 2013

Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema kuwa itakabidhi jukumu la ulinzi wa Afghanistan kwa nchi hiyo katikati ya 2013 pamoja na kutangaza kuanza mfumo wake mpya wa kinga ya makombora barani Ulaya utakaokamilika 2020.

Mkutano wa NATO mwaka 2012 , Chicago Marekani

Mkutano wa NATO mwaka 2012 , Chicago Marekani

Kutangazwa kwa hatua hiyo kumezusha hali ya kutoelewana baina ya NATO na Urusi ambayo imeendelea kusisitiza ipatiwe uhakika wa kisheria unaothibitisha kuwa mpango huo hauilengi nchi hiyo. Marekani yenyewe imeweka bayana shabaha yake katika mpango huo ni kuwa ni kujilinda dhidi ya Iran.

Akizungumza baada ya kutangazwa rasmi kwa mpango huo kwenye mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo unaoendelea mjini Chicago Marekani, Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa Urusi haina haja ya kuhofia hatua hiyo.

Baadae Rasmussen aliwaambia waandishi wa habari kwamba jumuiya hiyo ina lengo la kuendelea na mazungumzo na Urusi ikiwa na matumaini kuwa nchi hiyo itaielewa hatua yake hiyo kuwa ni sehemu ya mpango wake muhimu na wa muda mrefu katika kujihami na makombora

Mapema siku ya Jumapili Naibu Waziri wa Ulinzi wa Urusi Anatoly Antonov aliionya NATO kuhusu hatua hiyo ya kuendelea na mpango wake wa kutengeneza mfumo mpya wa kujikinga na makombora kwa nchi za ulaya akisema kitendo hicho kitavuruga amani ya dunia. Antonov alitishia pia kuwa nchi yake itachukua hatua za kijeshi kama mpango huo utaendelezwa.

Mpango wa kuondolewa vikosi vya NATO Afghanistan

Mkutano huo wa kilele wa NATO umezungumzia pia suala la kuondoka kwa vikosi vya kigeni vinavyolinda amani nchini Afghanistan ambapo maamuzi yaliyofikiwa ni kwamba nchi hiyo itakabidhiwa jukumu la kujilinda katikati ya mwaka 2013.

Mkutano wa NATO mwaka 2012 , Chicago Marekani

Mkutano wa NATO mwaka 2012 , Chicago Marekani

Katika siku yake ya pili leo, mkutano huo utajadili mbinu ya kuondolewa taratibu vikosi vyao nchini Afghanistan, kama ilivyopendekezwa na Marekani . Lengo ni kuziunganisha nchi zote zinazoshiriki katika kulinda amani nchini Afghanistan, kutimiza lengo hilo kwa pamoja baada ya Ufaransa kuonyesha nia ya kuviondowa vikosi vyake kabla ya muda uliopangwa mwaka 2014. Kufikia wakati huo vikosi vyenye jumla ya wanajeshi 130,000 vitakuwa vimeshaondoka.

Hata hivyo, Rais wa Ufaransa Francois Hollande baadae alitangaza kuwa amefikia makubaliano na wenziwe wa NATO kuhusu uamuzi wake wa kujiondoa mapema akisema wameelewa hali aliyonayo.

Hali ya kutaka kuziridhisha pande zote mbili

Nchi wanachama wa NATO wanataka kuwaonyesha wananchi wao wanaopinga serikali zao kujiingiza kwenye vita kuwa hali hiyo inafikia kikomo, lakini pia kwa upande mwingine wanataka kuwaambia Waafghan kuwa hawatawatelekeza.

Mataifa hayo yanapata upinzani mkali kutoka kwa wapiga kura ambao wanaona kuwa kujihusisha kwao kwenye vita hivyo kunazigharimu serikali zao kiuchumi.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai akizungumza na Rais Barack Obama wa Marekani.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai akizungumza na Rais Barack Obama wa Marekani

Kwa upande wake Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amesema kuwa anaisubiri siku ambayo nchi yake haitakuwa tena mzigo kwa jumuiya za kimataifa, kauli aliyoitoa wakati akizungumza na Rais Barack Obama wa Marekani pembezoni mwa mkutano huo.

Mwandishi: Stumai George/DPA/REUTERS/ AFPE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com