1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO kuimarisha mfumo wa amri na uwezo wa ulinzi kimtandao

John Juma
9 Novemba 2017

Wanachama wa NATO wakubaliana kuimarisha matumizi ya silaha na mikakati ya mitandao katika operesheni zao. Aidha mawaziri wa ulinzi wa jumuiya hiyo wakubaliana kuimarisha muundo wa amri na usafirishaji haraka wa majeshi

https://p.dw.com/p/2nKm2
Brüssel Treffen NATO-Verteidigungsminister | Mattis, USA & Stoltenberg, NATO-Generalsekretär
Picha: Getty Images/AFP/V. Mayo

Jumuiya ya Kujihami ya NATO itaimarisha muundo wake ili kuwezesha usafirishaji wa haraka wa majeshi kati ya eneo la Atlantiki na ndani ya Ulaya katika kukabiliana na ongezeko la kitisho cha Urusi. Hayo yameafikiwa na mawaziri wa ulinzi wa mataifa wanachama wa NATO wanaokutana mjini Brussels, ambao pia wamejadili uwezekano wa kuongeza juhudi kwenye vita vya mitandaoni.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, amesema uamuzi huo wa mawaziri unaakisi kujitolea kwa NATO kukabili changamoto zinazoibuka, na kwa hili itakuwa mara ya kwanza kwa jumuiya hiyo kuimarisha muundo wake wa amri tangu kumalizika kwa Vita Baridi.

Kituo kimoja cha amri kitaundwa kulinda mipaka ya baharini kote katika eneo la Atlantiki. Kingine kitalenga kuimarisha usafirishaji wa majeshi na vifaa ndani ya Ulaya.

Wito wa uimarishaji wa miundombinu Ulaya

Hatua hiyo inanuia kuzihimiza serikali za Ulaya kuimarisha miundombinu ndani ya nchi zao ili kuwezesha usafirishaji wa vifaa vizito kama vile magari ya kubeba silaha za kijeshi. Stoltenberg anaongeza: "Ni muhimu kwa NATO kushirikiana na Umoja wa Ulaya, na hakika tunafanya kazi kwa ukaribu na kwa ushirikiano kuhusu suala hili. Kwa mfano tunabadilishana taarifa kuhusu viwango, mahitaji na changamoto zinazohusiana na miundombinu ya kiraia."

Mpango wa kuimarisha uwezo wa kusafirisha majeshi ndani na nje ya Ulaya, unaonekana kama jibu kwa ongezeko la kitisho kutoka kwa Urusi. Kitisho kwa wanachama wa jumuiya hiyo kimezidi kuibua wasiwasi tangu Urusi kuichukua rasi ya Crimea mwaka 2014.

Afghanistan Kabul - NATO Soldaten erreichen Ort eines Selbstmordattentats
Picha: Reuters/M. Ismail

Matumizi ya mtandao katika makabiliano ya kijeshi

Japo Stoltenberg alisisitiza kuwa hatua za NATO hazilengi taifa lolote maalum na kuwa hakuna kitisho kikubwa dhidi ya nchi yoyote mwanachama wa NATO, alisema kuwa NATO imeiona Urusi ikijiongezea nguvu katika siku za hivi karibuni, ikiwemo kutumia nguvu za kijeshi nchini Ukraine. Wanachama wa NATO pia walikubaliana kuimarisha matumizi ya silaha na mikakati ya mitandao katika operesheni zao. Stoltenberg anasema

"Tumeona washirika wa NATO wamekuwa wakitumia uwezo wao kimtandao dhidi ya ISIS nchini Iraq na Syria na hiyo imekuwa muhimu katika vita dhidi ya ISIS. Na ninaamini sana kuwa katika vita makabiliano yoyote ya kijeshi, mtandao utakuwa kipengele muhimu na hivyo tunahitaji kuimarisha uwezo wetu wa kijeshi katika mitandao."

Vita vya Afghanistan na mzozo wa nyuklia wa Korea kaskazini kujadiliwa

Mawaziri hao wanakutana pia kujadili hatua za kuchukuliwa katika Afghanistan ambayo imekumbwa na machafuko kwa miaka 16. Mapema wiki hii, NATO ilitangaza kuwa itawatuma wanajeshi 3,000 zaidi nchini Afghanistan, na hivyo idadi ya wanajeshi kutoka magharibi walioko Afghanistan itaongezeka hadi 16,000.

Mzozo kuhusu silaha za nyuklia za Korea Kaskazini pia ni kati ya ajenda za mkutano huo ulioanza Jumatano na unaomalizika leo Alhamisi.

Mwandishi: John Juma/DPAE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef