Nani atasalimika katika kundi la kifo, Kundi B
7 Juni 2012Kwa baadhi itakuwa ni jinamizi, kwa wengine ni changamoto kubwa mno. Lakini katika suala moja wote wanakubaliana , kuwa kundi B la mashindano haya ni gumu mno. Nchini Denmark watu husema kuwa ni kundi "lenye miripuko", amesema hayo kocha wa kikosi cha Denmark Morten Olsen. Kundi hili linajumuisha timu za Ujerumani, Ureno, Denmark na Uholanzi.
Katika mashindano kama haya mwaka 1992 , Ureno, Uholanzi na Ujerumani zilikuwa katika kiwango cha pekee. Denmark inajiona kuwa haina chake katika kundi hili. Sisi ni wanyonge katika kundi hili. Hatuna nafasi kubwa, amesema mchezaji bora wa mwaka nchini Denmark William Kvist ambaye huchezea timu ya VfB Stuttgart nchini Ujerumani. Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw hata hivyo, anaiangalia Denmark kwa njia tofauti kabisa. Wadenmark huingia katika mashindano kama haya bila ya wasi wasi. Hawana woga na timu kubwa ama majina. Hali hii inawafanya wawe hatari zaidi.
Hata Ureno ingependelea kuwamo katika kundi rahisi kidogo. Kwa kuwa Ujerumani na Uholanzi zinaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi katika kundi hili. Hili ni kundi gumu kabisa , likiwa na timu tatu kubwa , ameeleza hayo kocha wa Ureno Paulo Bento.
Ugumu usingepaswa kuwapo, lakini mchezo wa kwanza timu hiyo inapaswa kupambana na Ujerumani. Timu hiyo makamu bingwa wa kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2004 inataka kulipa kisasi kwa kufungwa na Ujerumani katika mashindano yaliyopita ya kombe la Ulaya na kombe la dunia katika mwaka 2006. Ureno inaweza kuwa bingwa wa kombe la mataifa ya Ulaya, anasema nyota wa zamani wa Ureno Luis Figo.
Mara baada ya kupambana na Ureno , Ujerumani haitapumua kwani inakabiliana na mahasimu wao wa jadi Uholanzi. Tunajiamini , amesema kocha Löw. Wachezaji wanajisikia kuwa wako karibu na mafanikio makubwa. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel siku ya Jumatano(06.06.2012) alikula chakula pamoja na wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani siku tatu kabla ya kupambana na Ureno , katika Hotel Dwor Oliwski mjini Dazig nchini Poland. Merkel amesema kuwa nimehisi na kugundua kuwa kuna mshikamano na ari kubwa miongoni mwa wachezaji.
"Nimefurahi kwamba nimeweza kuja kuwatembelea . Nafahamu kuwa muda wa matayarisho kwenu mwaka huu umekuwa mfupi sana na natambua kuwa hilo mmelitilia maanani".
Kwa kupata matokeo mazuri katika michezo kumi ya kuwania kufuzu kucheza katika fainali hizi, timu hii inataka kutawazwa bingwa wa taji hili ambalo walilitwaa mwaka 1972, 1980 na 1996.
Uholanzi nayo inataka ubingwa wa kwanza baada ya miaka 24. Mwaka 1988 Uholanzi ilitawazwa bingwa wa mashindano haya,na tangu wakati huo Uholanzi haijafika hata katika fainali. Kikosi hicho chenye kiu kubwa ya kupata mabao cha kocha Bert van Marwijk kimefanikiwa bila matatizo kuingia katika fainali hizi na kupata mabao 37, manne zaidi ya magoli yaliyofungwa na Ujerumani katika hatua hiyo. Mstari wa ushambuliaji unaongozwa na Klaas-Jan Huntelaar na Robin van Persie. Lakini pamoja na hao wako nyota kama Wesley Sneijder, Arjen Robben na Dirk Kurt. Pamoja na kuwa na kikosi cha mauaji, lakini kocha van Marwijk anaheshimu timu katika kundi hili lenye miripuko.
Mwandishi : Olivia Fritz / ZR / Kitojo
Mhariri: Othman Miraji