1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani anayetawala Mali? Bado kitendawili

27 Septemba 2012

Miezi mitano baada ya Kapteni Amadou Sanogo kuyakabidhi rasmi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia, hali ya mkanganyiko bado inalitawala taifa la Mali juu ya nani hasa anayeiongoza nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/16GYE
Kapteini Amadou Sanogo aliyeongoza mapinduzi na rais wa mpito Dioncounda Traore
Kapteini Amadou Sanogo aliyeongoza mapinduzi na rais wa mpito Dioncounda TraorePicha: Reuters

Wanadiplomasia wanasema uchaguzi unahitajika kabla ya kuchukuliwa hatua ya kijeshi dhidi ya waasi wa kiislamu katika eneo la Kaskazini. Kauli hizo zinatolewa wakati kukionekana pia kuweko msuguano na hali ya kutofautiana kati ya viongozi wa serikali ya kiraia na mkuu aliyeongoza mapinduzi ya kijeshi.

Mvutano huo unawafanya wengi kujiuliza ni nani hasa kwahivi sasa anayeingoza nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mwanadiplomasia mmoja aliyeko mjini Bamako na ambaye hakutaka kutajwa jina anasema hakuna anayeidhibiti nchi hiyo kwa sasa kutokana na kuweko mpasuko ndani ya utawala wa mpito pamoja na hali ya kunyoosheana kidole kati yake na kambi ya kijeshi ya Sanogo juu ya sera muhimu za nchi hiyo.

Mvutano huo wa kisiasa mjini Bamako unawaghadhabisha waungaji mkono wa nchi hiyo kutoka Jumuiya ya Kimataifa huku ikijizatiti kuutafutia ufumbuzi mzozo mbaya kuwahi kuikabili tangu ijipatie uhuru wake.

---

Kuporomoka kwa demokrasia na uasi katika eneo lake la Kaskazini uliosababisha kundi la wanaofungamanishwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida kuchukua mamlaka ya thuluthi mbili ya eneo hilo ni masuala yaliyowashawishi nchi za Magharibi na nchi zenye nguvu katika eneo hilo la Afrika Magharibi kwamba panahitajika uchaguzi utakaoleta viongozi watakaochukua nafasi ya walioko serikalini waliogawika kabla ya nchi hizo kuamua kutuma kikosi cha wanajeshi cha Kimataifa kupambana na waasi kaskazini.

Hata hivyo hatua hiyo ya kuitishwa uchaguzi inaweza kusababisha harakati za kupeleka wanajeshi hao kufanyika mwaka ujao hali ambayo itatoa nafasi kubwa kwa waasi wa kiislamu ambao wanaharibu majengo ya kihistoria na kuwakata watu mikono wanaoshukiwa kuwa wahalifu kwa kuzingatia sheria ya Kiislamu,kujitanua na kupata nguvu zaidi ya kupenyeza mizizi ndani ya jamii pamoja na kusajili wapiganaji kutoka nje.

Waziri mkuu Cheick Modibo Diarra
Waziri mkuu Cheick Modibo DiarraPicha: Reuters

Maafisa wa Marekani wameshasema kwamba Mali ni lazima ifanye uchaguzi kabla ya harakati zozote za kulikomboa eneo la Kaskazini.

Rais wa Burkina Faso na ambaye ni msuluhishi wa mzozo wa Mali,Blaise Compaore akihojiwa wiki iliyopita na televisheni ya Ufaransa alitamka wazi kwamba hakuna utawala mjini Bamako.

Mwanadiplomasia mwengine wa ngazi ya juu mjini Bamako akisisitiza kauli ya Compaore akizungumza na shirika la habari la Reuters amesema msuluhishi huyo ametaja wasiwasi ambao pia upo katika Jumuiya ya Kimataifa. Anasema wanasiasa wa nchi hiyo wanabidi kushauriana na kuitisha uchaguzi utakaorudisha uhalali katika eneo la kaskazini.

Ameongeza kusema kwamba ni serikali halali pekee ndiyo inayoweza kulikomboa eneo hilo.Msemaji wa aliyekuwa kiongozi wa mapinduzi wa kijeshi Sanogo anasema hatua ya nchi za Magharibi ya kupinga harakati za kulikomboa eneo la Kakszini kabla ya uchaguzi haiwezi kukubalika akidai kwamba waasi wanasababisha kitisho cha Kimataifa.

Kwa upande mwingine wakosoaji wa rais wa mpito Diancounde Traore wanamshutumu kwa kuwa dhaifu na kushindwa kufanya kazi na waziri mkuu Cheick Modibo Diarra mtu ambaye anaonekana kujijengea himaya yake mwenyewe ya kisiasa na hilo ndilo jambo linalourefusha mzozo wa kisiasa mjini Bamako.

Aidha kutokana na mvutano huo serikali ya kiraia haina ushawishi na badala yake ushawishi unaonekana kutoka upande wa Sanogo mtu maarufu mjini Bamako ambako wengi wanashuku kwamba hataki kuachilia madaraka kikamilifu.

Ni wasiwasi huu wa kuweko kutoaminiani ndani ya serikali ya Mali ndiko kulikoifanya pia nchi jirani ya Guinea kuizuia meli ya silaha nzitonzito iliyokusudiwa kwenda Mali mwezi Julai ikisema inawasiwasi huenda silaha hizo zikaangukia kwenye mikono ya wasiostahili.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman