1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI:Serikali ya Somalia yahamia Mogadishu kutoka Baidoa

21 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCGn

Serikali ya muda ya Somalia imemaliza shughuli ya kuhamisha makao yake kutoka mji wa Baidoa hadi mji mkuu wa Mogadishu huku ghasia zikikumba eneo hilo.Hatua hiyo iliidhinishwa na bunge mwezi huu tarehe 12 .Hii ni mara ya kwanza tangu kuundwa kwa serikali hiyo ya muda kuhamia katika makao makuu ya Somalia.

Kulingana na balozi wa Somalia nchini Kenya Mohammed Nur Waziri Mkuu na baraza lake la mawaziri limeshahamisha makao yao huku bunge likisubiriwa kufanya hilo hivi karibuni baaada ya mkutano wa maridhiano kuandaliwa tarehe 16 mwezi ujao.

Waziri mkuu Mohammed Gedi anaripotiwa kushauriana na viongozi wa jamii ya Hawiye ambayo inapinga serikali hiyo ya

Muda ili wahudhurie kikao hicho. Kwa mujibu wa Balozi Mohammed Nur ghasia za hii leo zimesababishwa na msako wa wanamgambo wanaolaumiwa kutekeleza mashambulio katika mji wa Mogadishu.

Mjumbe wa Somalia nchini Kenya anaeleza kuwa serikali yake inapanga kuimarisha operesheni za usalama vilevile kusalimisha raia wa kawaida kufuatia ghasia zilizosababisha vifo vya takriban watu 14 hii leo.

Kulingana na wakazi wa eneo hilo mapigano makali yalizuka baada ya wanamgambo kushambulia makao ya majeshi ya Ethiopia yanayounga mkono jeshi la serikali ya Ethiopia.

Juhudi za kimataifa za kumaliza ghasia katika nchi hiyo zimeambulia patupu tangu Somalia kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya Mohammed Siad Barre kungolewa madarakani mwaka 91.