1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kidiplomasia wafukuta

23 Juni 2013

Mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na Ahmet Davutoglu wa Uturuki wamekutana Jumamosi (22.06.2013) kuzima mzozo wa kidiplomasia kuhusiana na suala la juhudi za Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/18uV5
Guido Westerwelle und Ahmet Davutoglu mjini Doha Qatar.
Guido Westerwelle und Ahmet Davutoglu mjini Doha Qatar.Picha: picture alliance/dpa

Mawaziri hao walikutana kwa mazungumzo mazito ya kubadilishana mawazo juu mzozo huo uliotokana na shutuma za Kansela Angela Merkel juu ya namna Uturuki ilivyokabiliana na waandamanaji na kusita kwake kutoa ridhaa yake katika mchakato wa Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Ujerumani na Uturuki hapo Ijumaa kila mmoja ilimwita balozi wa nchi moja kwa mwenzake kutaka ufafanuzi baada ya Merkel kusema amefadhaishwa kwa namna serikali ya Uturuki ilivyokabiliana na maandamano ya kupinga serikali na waziri wa Uturuki kumtuhumu kwa kukwamisha mazungumzo ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa sababu ya kutaka kujinufaisha kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao nchini mwake.

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema mazungumzo kati ya Guido Westerwelle na Ahmet Davotoglu yalifanyika pembezoni mwa mkutano wa juu ya mzozo wa Syria uliofanyika katika mji mkuu wa Qatar Doha. Imesema mazungumzo yao yamefanyika katika mazingira ya tija na urafiki na wamebadilishana mawazo mazito katika moyo wa ushirikiano na urafiki juu ya masuala yaliopo likiwemo suala la uhusiano wa Uturuki na Umoja wa Umoja wa Ulaya na uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Mzozo wa kidiplomasia wafukuta

Mjini Ankara mji mkuu wa Uturuki balozi wa Ujerumani Eberhard Pohl alikuwa na mazungumzo na naibu waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Feridun Sinirlioglu katika wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo hapo Jumamosi.Kutokana na kubadili mawazo kwa Ujerumani dakika za mwisho Umoja wa Ulaya unatazamiwa kuahirisha au kufuta mipango ya kufunguwa ukurasa mpya wa mazungumzo ya kujiunga na Umoja wa Ulaya yaliokuwa yamepangwa kufanyika Jumatano ijayo.

Maandamano ya kupinga serikali nchini Uturuki mwezi wa Juni mwaka 2013.
Maandamano ya kupinga serikali nchini Uturuki mwezi wa Juni mwaka 2013.Picha: Reuters

Uturuki imeishutumu Ujerumani kwa kukwamisha kuanza kwa mazungumzo hayo wakati wa mkutano wa Brussels uliofanyika Alhamisi. Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zilishindwa kufikia muafaka katika kufunguwa ukurasa mpya wa mazungumzo ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya jambo ambalo lingeliimarisha uhusiano na umoja huo. Uholanzi pia imepinga kuanza kwa mazungumzo hayo.

Waziri anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya wa Uturuki Egemen Bagis alifoka hapo Alhamisi kwamba kugoma kwa Ujerumani kuanza kwa mazungumzo ya Uturuki kunahusiana na suala la kampeni ya uchaguzi ya Kansela Angela Merkel.

Ujerumani yaonywa

Awali alionya kwamba Ujerumani itakabiliwa na hatua za kujibu mapigo iwapo Merkel hatoachana na pingamizi lake hilo.Bagis aliwaambia waandishi wa habari anatarajji Merkel atasahihisha kosa alilofanya kufikia Jumatatu venginevyo jambo hilo litasababisha Uturuki ichukuwe hatua.Mapema wiki hii alimtaka Merkel afikirie faida inazopata takriban kampuni 4,000 za Ujerumani zilioko Uturuki.

Waziiri wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya Egemen Bagis.
Waziiri wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya Egemen Bagis.Picha: AP

Bagis hapo Alhamisi moja kwa moja aliitwisha lawama Ujerumani taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi katika Umoja wa Ulaya na yenye idadi kubwa ya jamii ya Waturuki nchini mwake halikadhalikia ikiwa pia ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Uturuki.

Bagis amesema "Iwapo Merkel anatafuta maudhui ya kampeni yake ya uchaguzi, haipaswi kuwa Uturuki" akimaanisha uchaguzi mkuu wa Ujerumani uliopangwa kufanyika hapo mwezi wa Septemba.

Mazungumzo yako mashakani

Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zinaunga mkono kuanza kwa mazungumzo zaidi na Uturuki katika mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya wiki ijayo. Zinasema kwamba uchumi wa Uturuki unaokuwa kwa haraka,idadi yake kubwa ya vijana na ushawishi wake wa kidiplomasia utaimarisha Umoja wa Ulaya.

Bendera nyekundu ya Uturuki ikipepea bega kwa bega na ile ya Umoja wa Ulaya.
Bendera nyekundu ya Uturuki ikipepea bega kwa bega na ile ya Umoja wa Ulaya.Picha: AP

Wakati hali ya mvutano kati ya Ujerumani na Uturuki ilipokuwa ikipamba moto waziri wa mambo ya nje wa Italia Emma Bonino amesema huu sio wakati wa kuifungia milango Uturuki lakini hakuitaja moja kwa moja Ujerumani.

Wahafidhina wa Merkel wanapinga uwanachama wa Uturuki kwa Umoja wa Ulaya katika ilani yao ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi wa Septemba kwa kusema itaielemea Umoja wa Ulaya kutokana na ukubwa wa nchi hiyo na uchumi wake juu ya kwamba Merkel amesita kutowa wito wa moja kwa moja wa kutaka kusitishwa kwa mazungumzo hayo ya mchakato wa Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri: Caro Robi