1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Catalonia wafika Ujerumani

Josephat Charo
26 Machi 2018

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamejishughulisha na kutiwa mbaroni kwa Carles Puigdemont, maandamano ya kupinga silaha Marekani, na machungu ya kisiasa aliyoyapata Martin Shulz.

https://p.dw.com/p/2uyKu
Carles Puigdemont
Carles Puigdemont, kiongozi wa zamani wa CataloniaPicha: Reuters/Lehtikuva/M. Kainulainen

Mzozo wa Catalonia umeshawasili mjini Berlin. Wasiwasi mkubwa umeibuka. Hata hivyo mhariri anatilia maanani kwamba kuna umoja katika serikali ya mseto mjini Berlin, kwamba msimamo wa wanaharakati wa Catalonia wanaotaka kujitenga si halali kisheria na wala haukubaliki. Bila shaka kuna uwezekano mataifa mengine ya Ulaya yakajiuliza, je Uhispnaia inajaribu kulisambaratisha vuguvugu la demokrasia kupitia jela na faini? Ni suala lililo bayana kwamba idara ya mahakama ya Uhispania inapania kuuvuruga mfumo wa kijamii na kiuchumi wa wanaharakati wa Catalonia.

Mhariri anasema suala hili haliwahusu magaidi, bali wanasiasa waliochaguliwa kihalalai katika uchaguzi huru, ambao wanatumia njia za amani kujitetea. Mpaka sasa makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels hayajaingilia kati kuwapatanisha viongozi wa Barcelona na waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo uliopo. Sasa serikali ya Ujerumani inalazimika kuchukua jukumu hilo.

Nalo gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger kuhusu Puidgedemont linasema waasi wa Catalonia hawakuzingatia hasira na nguvu ya taasisi za Uhispania. Mhariri wa gazeti hilo anasema waasi hao wameshindwa vita na Catalonia inabakia sehemu ya Uhispania. Huu ungekuwa wasaa mwingine wa kila mtu kufanya tena siasa. Vyama vya waasi wanaotaka kujitenga, ambavyo vina wingi katika bunge la jimbo la Catalonia, vinatakiwa kuunda serikali itakayoweza kusimamia mazungumzo haraka iwezekanavyo na ambayo inatambua ukweli halisi wa mambo yalivyo. Na wengine wote wanatakiwa kujiepusha na hamasa za kutaka kuendelea kuwashinda waasi ambao tayari wameshashindwa.

Maandamano ya kupinga silaha Marekani

Mada ya pili iliyozingatiwa na wahariri inahusu maandamano ya wanafunzi wa shule ya Parkland jimboni Florida kutaka hatua zichukuliwe kudhibiti silaha nchini Marekani. Gazeti la Frankfurter Rundschau limeandika: Wanafunzi wa Parkland walishuhudia jambo la kutisha sana katika uvamizi wa mwezi uliopita, lakini huzuni na ghadhabu yao imewabadilisha na kuwa vuguvugu lenye nguvu ambalo linastahiki heshima.

Washington  March For Our Lives Protestmarsch
Maandamano ya mjini WashingtonPicha: Getty Images/A. Wong

Mhariri anatilia maanani kwamba chama cha wamiliki wa silaha na makundi ya ushawishi bado hayajashindwa. Wanaharakati hao vijana watahitaji kuvuta pumzi. Watafaulu tu kuleta mabadiliko iwapo harakati zao zitageuka kuwa kura katika chaguzi za bunge. Kwa upande mwingine maandamano dhidi ya umiliki wa silaha huenda yakaleta matokeo hasi: Inawezekana hadi kufikia uchaguzi wa Novemba, suala la umiliki wa silaha likawa mada nyingine ya umuhimu itakayozingatiwa ukiacha mbali mzozo wa Iran na sera ya uhamiaji.

Naye mhariri wa gazeti la Südwest Presse kuhusu mada hii anasema maandamano haya aliyofanyaika Washingon na maeneo mengine ya Marekani yamedhihirisha kwamba vijana wa Marekani pia wamo katika siasa. Tofauti iliyopo ni jinsi wanavyofanya siasa. Wanajikita zaidi katika miradi. Wanaharakati hawa wapya wa kisiasa hawafuatiliii malengo yasiyoweza kufikiwa. Ndio maana maandamano hayakutaka umiliki wa silaha upigwe marufuku, maana wanafahamu fika hilo haliwezekani. Lakini wamechukua mkondo tofauti unaoonekana kuwa wa kisiasa zaidi ikilinganishwa na mavuguvugu mengine ya vijana ya miongo iliyopita. Mhariri anamalizia kwa kusema hiyo ni ishara ya matumaini.

Masaibu yaliyomkabili Martin Schulz katika siasa

Tunakamilisha na gazeti la Trierischer Volksfreund linalozungumzia kuhusu makali ya kisiasa yaliyomkuta mgombea wa zamani wa ukansela wa Ujerumani wa chama cha Social Democratic, SPD, Martin Schulz. Mhariri wa gazeti hilo anasema Martin Schulz ndiye mwanasiasa pekee aliyeonja, katika kipindi cha mwaka mmoja ni jinsi gani siasa zinavyoweza kuwa na machungu makubwa na bila huruma.

Deutschland schlafende Politiker Andrea Nahles
Martin Schulz (kushoto)Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Aliabudiwa kama Mungu na chama cha SPD lakini baadaye akatimuliwa na kufukuzwa kama mtu aliyeshindwa. Lakini masaibu yake kisiasa hayajaja tu kama janga la kiasili. Hilo ameliona mwenyewe huyo Schulz. Wakati wa kampeni za uchaguzi na hata baada ya uchaguzi wa Ujerumani, Schulz alifanya makosa mengi. Hatimaye matokeo ya yeye kujiuzulu nyadhifa zote, mhariri anasema, ni jambo muhimu lililohitajika.

Mwandishi: Josephat Charo/Inlandspresse

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman