1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo katika masoko ya fedha duniani

Othman, Miraji16 Septemba 2008

Mzozo wa mabenki Marekani waleta vurugu katika masoko ya fedha duniani

https://p.dw.com/p/FJ6D
Waziri wa fedha wa Marekani, Henry PaulsonPicha: AP

Bei za hisa za makampuni makubwa duniani leo zimezidi kwenda chini kwa siku ya pili mfululizo, huku wawekezaji walio na wasiwasi wanangojea ikiwa kampuni kubwa la bima huko Marekani, AIG, litafilisika kama ilivyotokea kwa benki kubwa ya Lehmann Brothers. Katika biashara ya leo asubuhi, bei za hisa za makampuni hapa Ulaya zilikwenda chini, baada ya masoko ya fedha kupata mtikiso mkubwa huko Asia na pia Marekani. Na kutokana na mzozo unaosamabaa katika masoko ya fedha ya Marekani, waziri wa fedha wa Marekani, Henry Paulson, ametoa mwito watu wawe na imani juu ya uchumi wa nchi yake.

Kila mambo yanavozidi kuwa mabaya, ndivyo waziri huyo wa fedha wa Marekani anavozidi kuwa hana wasiwasi. Hajataka kuwasikiliza wale watu walioitaja siku ya jana ya msukosuko mkubwa katika masoko ya fedha duniani kuwa ni jumatatu nyeusi. Alishikilia kwamba mfumo wa mabenki ya Marekani ni imara na thabiti, ila tu ni wakati sasa kwa masoko ya fedha ya nchi yake kusafishwa baada ya mabenki, kutokana na kutokuwa na dhamana katika kutoa mikopo, imeyaharibu masoko ya mikopo ya nyumba na pia kujiumiza yenyewe. Alisema:

" Tutauvuka mzozo huu sio kwa siku moja na sio bila ya mishtuko mikubwa.+

Wazrii Henry Paulson aliweka wazi kwamba walipaji kodi wa nchi yake walizuwia kuporomoka benki ya uwekezaji ya Bear Stears na kusambaratika shirika la kutoa mikopo ya nyumba la Fanny na Freddy. Lakini alisisitiza kwamba haijamjia akilini hata kidogo kwamba sasa azitie hatarini fedha za walipa kodi wa Kimarekani ili kuokoa kufilisika benki ya Lehman Brothers. Alisema ulikuwa mtindo uliopitwa na wakati kwamba inapopatikana faida, basi hiyo iwe ni faida ya watu binafsi, lakini pale inapopatikana hasara, basi hasara hiyo ibebwe na jamii.

Naye mtetezi wa chama cha Republican katika uchaguzi wa urais huko Marekani, John McCain, aliwalaumu mameneja wa benki zilioko katika Wall Street huko Marekani kuwa wanaendesha biashara kama vile wacheza kamari. Aliahidi kwamba pindi chama chake cha Republican kitabakia madarakani, basi atachukuwa hatua za haraka, na mambo kuwa vingine katika mabenki.

"Naahidi tutayasafisha mabenki yalioko huko Wall Street."

Naye mshindani wa McCain katika uchaguzi wa urais, Barack Obama wa Chama cha Democratic, alisema Chama cha Republican kilikuwa na miaka minane kuyasafisha mabenki ya uwekezaji. Alisema siasa za kiuchumi za Chama cha Republican zimesababisha mzozo mkubwa kabisa wa kifedha tangu kile kisa kikubwa cha kuporomoka Uchumi wa Marekani katikamwaka 1929. Mzozo huu wa sasa wa mabenki huko Marekani unawaumiza zaidi wafanya biashara wadogowadogo na zile biashara mpya ambazo hazijatimia zaidi ya miaka mitano tangu kuanzishwa. Makampuni hayo sasa hayatapata mikopo zaidi, japokuwa makampuni hayo yanaunda asilimia hamsini ya nafasi za kazi.

Hata hivyo, kuna matarajio kidogo kwa maelfu ya wafanya kazi wa Benki ya Lehman Brothers walioachishwa kazi, kwani benki ya Uengereza ya Barclays imesema inafanya mazungumzo juu ya uwezekano wa kununua baadhi ya mali za kampuni hiyo ya Kimarekani iliofilisika.Kuna uwezekano wa wafanya kazi 10,000 wa benki hiyo kuhamishiwa katika benki ya Barclays.