1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwili wa makamu wa rais wa chama cha upinzani nchini Rwanda wapatikana

Kabogo Grace Patricia14 Julai 2010

Mwili huo wa Andre Kagwa Rwisereka umepatikana karibu na gari lake lililokuwa limetelekezwa.

https://p.dw.com/p/OJE4
Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: picture-alliance/dpa

Mwili wa Makamu wa Rais wa chama cha upinzani ambacho hakijasajiliwa nchini Rwanda cha Democratic Green, Andre Kagwa Rwisereka, hatimae umepatikana karibu na gari lake. Rwisereka alikuwa hajulikani alipo baada ya gari lake kukutwa limetelekezwa karibu na mji wa Butare. Haya yametokea wakati kukisalia wiki chache kabla ya uchaguzi wa rais nchini humo mwezi ujao.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi pamoja na chama cha Democratic Green imethibitisha kupatikana kwa mwili wa Bwana Rwisereka aliyetangazwa kutojulikana alipo mapema jana. Gari la makamu huyo wa rais wa chama hicho cha upinzani lilikutwa karibu na mto Mukula mjini Butare. Msemaji wa polisi Eric Kayiranga amesema mwili wa Bwana Rwisereka umepatikana majira ya asubuhi ya leo umbali wa kilometa tatu kutoka eneo ambako gari lake lilionekana, huku kukiwa na kisu kikubwa kinachodhaniwa ndicho kilitumika katika mauaji yake. Kayiranga amesema watu waliomuona usiku kabla ya kutoweka wamesema alikuwa na fedha nyingi, hivyo wanahisi huenda lilikuwa ni tukio la ujambazi na kwamba uchunguzi wa tukio hilo tayari umeshaanza. Msemaji huyo wa polisi amesema mwili huo umekutwa ukiwa na majeraha kifuani na umepelekwa hospitali.

Bwana Habineza amesema chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana na kwamba sasa na yeye anaishi kwa woga kwa sababu hapo awali alishawahi kupokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana. Chama cha Democratic Green kimekuwa kikishindwa kupata usajili utakaokiwezesha kushiriki katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwezi ujao. Kwa upande mwingine mashirika ya kutetea haki za binaadamu yameilaumu serikali ya Rwanda kwa kukandamiza wapinzani pamoja na vyombo vya habari kuelekea kwenye uchaguzi huo. Aidha, Rwanda imekanusha tuhuma hizo ikisema kuwa serikali imekuwa ikifanya mazungumzo na kukubaliana na baadhi ya maoni ya wapinzani tangu yalipotokea mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Hata hivyo, polisi nchini Rwanda wamemkamata mwandishi habari wa kujitegemea kwa tuhuma za kumfananisha Rais Paul Kagame na kiongozi wa Manazi a Ujerumani, Adolf Hitler. Polisi imelithibitisha hilo, ingawa afisa wa polisi amekanusha kuwa kukamatwa kwake kunahusiana na uchaguzi mkuu ujao. Msemaji wa polisi nchini Rwanda, Eric Kayiranga alisema kuwa Saidati Mukabibi, mwandishi wa gazeti la kujitegemea la Umurabyo alikamatwa kwa kosa la kukashifu, kuvuruga usalama wa nchi na ubaguzi wa kikabila. Baraza la habari la Rwanda-MHC limesema kukamatwa kwa Mukabibi hakuhusiani na uchaguzi ujao, ambao Rais Kagame anategemewa kushinda kwa kupata wingi wa kura.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman