1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenge wa Olimpik San Francisco

9 Aprili 2008

Wakereketwa 7000 kuandamana leo San Francisco pale mbio za mwenge wa olimpik zikianza.

https://p.dw.com/p/DemI

Maalfu ya waandamanaji watajipanga usiku wa leo katika barabara za mji wa San Francisco,Marekani pale mwenge wa Olimpik utakapopita huko ukielekea Beijing-kituo cha michezo ya mwaka huu ya Olimpik hapo Agust 8.

Kiasi cha waandamanaji 7,000 wanatarajiwa huku ulinzi mkali usiowahi kuonekana ukiwekwa na vikosi vya usalama.Tayari jana katika maombolezi maalumu,askofu desmond Tutu wa Afrika kusini,mshindi wa Tuzo la amani la Nobel, alitoa mwito wa kususiwa michezo ya Beijing kwa kuwa china inakanyaga haki za watibeti.Pamoja nae alikuwa mcheza-cinema mashuhuri na mkereketwa wa Tibet Richard Gere.

►◄

Vikundi mbali mbali vya wakereketwa vimewasili San Francisco,California kwa safari ya mwenge wa Olimpik unaoelekea Beijing kupitia miji mbali mbali ulimwenguni pamoja na Dar-es-salaam,jumapili hii.

Mbio za kuupitisha mwenge huo zitaanza saa 7 mchana saa za huko-kiasi cha saa 4 usiku-saa za Afrika mashariki.

kabla zahama zinazotazamiwa kuukabili mwenge huo baadae leo , kiasi cha waandamanaji na wakerteketwa 2000 walishiriki katika mkesha maalumu wa kuasha mishumaa mjini San Francisco,hafla ambayo ilihudhuriwa na mshindi wa tuzo la amani la Nobel,askofu Desmond Tutu wa Afrika kusini na nyota ya Hollywood-mcheza cinema maarufu richard Gere.Kiasi cha waandamanaji 800 waliandamana hadi kwenye Ubalozi mdogo wa China wakipaza sauti " AIBU KWA CHINA" na "IACHIE HURU TIBET SASA HIVI".

Maandamano haya ni tokeo muhimu sana -alisema mwanacinema huyo Richard Gere,mwenyekiti wa kampeni ya kimataifa kwa Tibet. Gere akasema,

"Jamii ya utulivu na maskizano ambayo rais Hu Jintao wa china anayozungumzia ni udanganyifu mtupu.Kwani, hakutawezekana kuwapo maskizano na utulivu bila kuwapo uhuru wa kuabudu na utamaduni."

Mmoja kati ya wakereketwa hao katika maandamano ya jana huko San Francisco alisema:

"Tibet imekaliwa na China kinyume na sheria kwa kiasi cha miaka 50.Katika kipindi hicho kumekuwapo utawala muovu,matumizi ya nguvu na kuwakandamiza wananchi wa Tibet."

Mkereketwa mwengine ambae licha ya malalamiko na vilio vya kudai michezo ya Olimpik ya Beijing isusiwe, anapanga kuhudhuria pamoja na mjukuu wake anasema:

"Nafikiri China, inajaribu kuonesha ni raia mwema wa dunia hii na ninapanga pamoja na mjukuu wangu kwenda katika michezo ya Olimpik ya Beijing na tayari ameshapata mwenge mdogo wa Olimpik."

Wakereketwa wa Tibet wameuandama mwenge wa olimpik tangu awali ulipoashwa katika nchi ya asilia ya Olimpik-Ugiriki hapo Machi 24 huku waandamanaji wakiituhumu China, mwenyeji wa michezo hiyo kukiuka haki za binadamu na kwa kutumia mkomoto huko Tibet.Wanadi kuwa hadi watibet 150 huko wameuwawa.

China kwa upande wake inasema 'wafanyaji machafuko" wameua watu 20.

Halmashauri kuu ya olimpik Ulimwenguni (IOC) imearifu kwamba inaendelea kuangalia safari ya mwenge huo kufuatia maandamano na fujo zilizozuka mjini London na Paris .

Hatahivyo, IOC haitii maanani sana fikra za kuivunja mila ya mwenge wa olimpik na safari yake ya maili 85,000 ilioanzia karne ya 20.

Rais wa Halmashauri Kuu ya olimpik ulimwenguni -mbelgiji Jacques Rogge akizungumza kabla kikao cha siku 2 kinachoanza kesho mjini Beijing cha halmashauri yake tendaji,amesema maandamano yasiruhusiwe kupotosha njia ya mwenge .

Thomas Bach,makamo-rais wa IOC kutoka Ujerumani mbio za kupokezana mwenge zisonge mbele licha ya maandamano ya wakereketwa.Kwa jicho hilo,mwenge wa olimpik watazamiwa kuwasili Dar-es-salaam,kituo pekee barani Afrika jumapili hii.