1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanzo mpya kwa Libya

22 Agosti 2011

Utawala wa Muammar Gaddafi wa Libya uko ukingoni kabisa wa kuporomoka. Kwa mujibu wa vyombo vya habari ni kwamba waasi wameshaidhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Tripoli.

https://p.dw.com/p/12LOF
Rais Muammar al-Gaddafi wa Libya yuko katika ncha ya ukingoni kabisa ya utawala wakePicha: AP

Utawala wa Muammar Gaddafi wa Libya uko ukingoni kabisa wa kuporomoka. Kwa mujibu wa vyombo vya habari ni kwamba waasi wameshaidhibiti sehemu kubwa ya  mji mkuu wa Tripoli. Habari hiyo ni nzuri, anasema Rainer Sollich wa Idara ya Kiarabu ya Deutsche Welle katika uhariri wake. Unasomwa studioni na Othman Miraji...

Licha ya kutojulikana yale yatakayotokea, alama zilioko za mwisho wa utawala wa Muammar Gaddafi ni za kufurahisha. Hivyo, unamalizika utawala wa kikatili na wa mabavu uliodumu miaka 42. Walibya wana haki ya kuwa na uhuru na kuweza kujiamulia wenyewe mustakbali wao. Wana haki ya kuwa na maisha ya heshima, bila ya mateso, bila ya kudang'anywa na kukandamizwa. Na wao, kwa ujasiri mkubwa na kujitolea mhanga kukubwa, wameipigania haki hiyo.

NATO Angriffe auf Tripolis Libyen Gaddafi
Mashambulio ya ndege za kijeshi za NATO katika mji mkuu wa Libya, TripoliPicha: dapd

Bila ya msaada wa kutoka nchi za Magharibi, mafanikio ya kijeshi ya waasi yasingwezekana. Mashambulio ya angani ya mabomu yaliofanywa na jeshi la NATO yamewawezesha waasi hao kusonga mbele. Hiyo, lakini, haipunguzi mafanikio walioyapata waasi, ambapo bila ya msaada huo wa NATO wangekuwa hawana matumaini. Lakini hali hii ya sasa inahitaji pia Walibya wawe na dhamana kubwa. Kujengwa demokrasia na jumuiya za kiraia katika Libya litakuwa ni jambo gumu zaidi kuliko ilivyo huko Tunisia na Misri, kwani chini ya Gaddafi, katika nchi hiyo hakujakuweko vyama vya kisiasa na taasisi za dola zinazofanya kazi. Kwa hivyo, nchi hiyo itabidi kikweli ianze kutoka sufuri. Ushauri mzuri ni kwa nchi za Ulaya kutoa msaada katika mambo hayo. Watawala wa mabavu huko Tripoli katika muda uliopita mara nyingi walidanganyika kutokana na mawazo ya watu wengine kuitilia maanani hali halisi ya kisiasa, na kwa hivyo watawala hao wakasahau kwamba wanawakandamiza watu wao.

Dhamana kubwa sasa wanaibeba wenyewe Walibya. Mapambano yao yamedhihirisha kwamba mtawala wa mabavu, ikiwa dharura, anaweza pia kushindwa kwa njia ya silaha. Hali hiyo pia itawapa mori wapinzani wa tawala za huko Syria, Yemen na nchi nyingine. Wao wanapigania haki hizohizo, na pia wanastahiki kupewa msaada ulio bora kabisa wa nchi za Magharibi. Walibya lazima sasa wadhihirishe kwamba kwa pamoja wanaweza kujenga mustakbali wao. Hatari zilioko mbele yao zisidharauliwe, kwani uwezekano wa kutokea mizozano ndani ya jamii ni mkubwa. Vitendo vya kikatili vya kulipiza visasi dhidi ya wafuasi wa utawala wa zamani visiwekeo kabisa, kwani hiyo itakuwa sumu kwa mwanzo mpya. Na upinzani uliogawanyika lazima ujipange katika vyama vya kisiasa. Makabila lazima yachanganyishwe na kuweko wizani sawa wa maslahi. Katiba mpya ni muhimu kuweko, chaguzi za kidemokrasia lazima zitayarishwe kwa uzuri.

Hayo yote yanaweza kuchukuwa wakati, na kama ilivyoonekana huko Misri, yanaweza kupelekea matokeo ambayo nchi za Ulaya zisingependa kuyaona- kama vile kuchomoza vyama vya Kiislamu vilivo na nguvu. Ikiwa mambo yatakuwa mazuri, Libya inaweza kuwa mfano mzuri wa ushirikiano baina ya Ulaya na nchi ya Kiarabu katika eneo la Bahari ya Mediterranean. Na ni pale Ulaya itakapoweza, kwa mafanikio, kuunga mkono mwenendo wa dimokrasia katika Libya, bila ya kujitia kimbelembele katika mambo ya siasa ya nchi hiyo. Ujerumani, kwa makusudi, haijashiriki katika harakati za kijeshi dhidi ya Gaddafi. Litakuwa jambo linalofaa kufikiriwa kwamba pia katika siku za mbele Ujerumani ichangie vikubwa katika ushirikiano wa kisiasa na Libya.

Mwandishi: Rainer Sollich/ Othman, Miraji/ZR

Mhariri:  Mohammed Abdulrahman