1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

mwaka 2007 ulikuwa mbaya kwa waandishi wa habari

Scholastica Mazula5 Februari 2008

Kwa waandishi wa habari ulimwenguni kote, mwaka jana kilikuwa ni kipindi kigumu zaidi ya muongo mmoja uliopita.

https://p.dw.com/p/D317

Kwa waandishi wa habari ulimwenguni kote, mwaka jana kilikuwa ni kipindi kigumu zaidi ya muongo mmoja uliopita.Taarifa hizi ni kwa mujibu wa kamati ya kutetea haki za waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari, CPJ.

Ikiwasilisha taarifa yake ya mwaka, iliyopewa jina la "Ugaidi katika habari", kamati hiyo imetoa shutuma kwamba Serikali katika nchi nyingi zimeongeza ukandamizaji dhidi ya wandishi wa habari.

Dave Marash, mwandishi wa habari wa Televisheni amenukuliwa akisema kwamba katika asilimia themanini na tano ya visa vyote hakuna mashitaka yaliyofunguliwa dhidi ya washitakiwa na hii inaleta hali ya hatari zaidi kwa wandishi wa habari.

CPJ; imetoa wito kwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, kuzishinikiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuheshimu uhuru wa Vyombo vya habari.

kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na CPJ, unaonyesha kwamba kiasi cha wandishi wa habari sitini na tano waliuawa katika kipindi cha mwaka jana katika matukio ambayo yanahusishwa na kazi zao.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka vifo vya wandishi hamsini na sita kwa taarifa ya mwaka jana, na kamati hiyo inaendelea na uchunguzi kwa wandishi ishirini na mbili kujua kama vifo vyao vinahusiana na kazi.

kwa mujibu wa CPJ, mwaka 1994 ulikuwa ni mwaka wa hatari zaidi wakati ambapo wandishi sitini na sita waliuawa na wengi wao walikuwa wakifanya kazi katika nchi ambazo zilikuwa na migogoro kama vile Nigeria, Bosnia na Rwanda.

Aidha taarifa hiyo inafafanua kwamba Iraq ni moja ya nchi ambazo zinaifanya kazi ya habari kuwa ngumu zaidi, kwani kwa kipindi cha miaka mitano, Iraq imebakia kuwa eneo hatari kwa wandishi wa habari kwa sababu kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka jana kulikuwa na waathirika wa hali hiyo thelethini na moja.

Kamati hiyo ya kutetea haki na uhuru wa wandishi wa habari imesema kwamba , waandishi wengi wa habari waliopoteza maisha yao nchini Iraq akiwemo mwandishi wa habari wa Washington Post Salih Aldin ambaye alifariki mjini Baghdad kutokana na kupigwa risasi kichwani mwake.

Uchunguzi unaonyesha kuwa vifo vya wandishi ishirini na nne vilivyotokea mwakia jana, yalikuwa ni mauaji yaliyopangwa, ikiwemo mashambulio ya kujitoa mhanga na juhudi zinazofanywa na Marekani zinawaweka wandishi wa habari kuwa katika hali ya hatari zaidi.

Miongoni mwa waandishi thelethini na moja waliouawa nchini mmoja kati yao alikuwa ni raia wa Iraq, lakini kwa mujibu wa CPJ, mwaka 2007 ni bora zaidi ya mwaka 2006 ambapo waandishi thelethini na mbili walipoteza maisha yao.

Hata hivyo katika uchunguzi huo CPJ, haikutoa idadi ya waandishi waliouawa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita hadi mwaka 2006. Kwa upande wa mwaka 2007 hali inaonyesha kwamba kulikuwwa na vifo vya waandishi wawili waliouawa nchini Eritrea na mmoja nchini Zimbabwe.

Hakukuwa na mauaji ya waandishi nchini Colombia na mauaji ya kwanza nchini humo yalikuwa miaka kumi na tano iliyopita.Na kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1999 hakujawahi kutokea mauaji ya waandishi yanayohusishwa na kazi ya uandishi nchini Ufilipino.

Mwezi Novemba mwaka jana CPJ, ilifanikiwa kuanzisha kampeni kupinga uonevu na kudai haki katika mauaji ya waandishi wa habari.

Kampeni hiyo ililengwa zaidi katika nchi za Ufilipino na Russia, ambazo ni miongoni mwa nchi zilizokuwa hatari kwa waandishi katika kipindi cha miaka kumi na tano iliyopita.

Mmoja wa wajumbe walioko katika kamati ya CPJ, Simon, anasema kwamba katika kila nchi ulimwenguni, waandishi wa habari wanaoandika habari za ukosoaji au habari muhimu, mara nyingi hunyamazishwa.

Akinukuu katika nchi za Pakistani na Sri Lanka, anasema kwamba waandishi wa habari watano waliuawa kutokana na kazi zao,kwa mfano mwaandishi Muhammad Arif, wa shirika la habari la ARY; na waandishi wengine wawili walipoteza maisha yao kutokana na mabomu ya kujitoa mhanga.

Hata hivyo CPJ, inaamini kwamba kuongezeka kwa msukumo wa kimataifa kuhusu waandishi wa habari, kutasaidia kubadilisha mtazamo wa Serikali wa kuwanyamazisha waandishi, kwa wale ambao hukwepa tuhuma za kweli na kukimbilia kuvishitaki vyombo vya habari.