Musharraf alikataa takwa la Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Musharraf alikataa takwa la Marekani

Rais Pervez Musharraf amelikataa takwa la Marekani linalomtaka amalize utawala wa hali ya hatari nchini Pakistan. Sambamba na hayo, polisi wamewakamata viongozi zaidi wa upinzani kwenye maandamano ya kumpinga rais Musharraf.

Jenerali Pervez Musharraf

Jenerali Pervez Musharraf

Rais wa Pakistan, jenerali Pervez Musharraf, amelitakaa ombi la Marekani linalomtaka amalize utawala wa hali ya hatari akisema aliitangaza hali hiyo ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwakani, unafanyika kwa amani na utulivu.

Jenerali Musharaf mwenye umri wa miaka 64, amekuwa akishinikizwa na Marekani arejeshe utawala wa kidemokrasia nchini Pakistan. Rais Musharraf ameukataa mwito uliotolewa na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, unaomtaka amalize utawala wa hali ya hatari alioutangaza mnamo tarehe 3 mwezi huu wa Novemba.

Jaji wa zamani wa mahakama kuu ya Paksitan, Wajihuddin Ahmad amesema, ´Kwa mtazamo wa Pervez Musharraf si kosa. Kwa mtazamo wa Benazir Bhutto ni kosa. Ni kosa pia kwa mtazamo wetu. Hii imesababisha mgawanyiko katika upande wa upinzani ambao unatakiwa uungane. Ikiwa unataka kumuondoa dikteta, upinzani lazima uungane.´

Rais Musharraf amesema kwamba amri ya hali ya hatari nchini Pakistan ni ya haki kwa sababu mahakama kuu ilijiingiza sana katika maswala ya kisiasa, hususan kuhusu kuchaguliwa kwake tena na sababu ya tisho kubwa kutoka kwa magaidi.

Ukaidi wa rais Musharraf umejitokeza siku chache baada ya rais George W Bush wa Marekani kumwambia wazi katika mazungumzo ya simu afanye uchaguzi kama ilivyopangwa na pia ajiuzulu wadhifa wake jeshini. Rais Bush alisema haiwezekani Pervez Musharraf awe rais na wakati huo huo kamanda mkuu wa jeshi la Pakistan.

Tume ya uchaguzi ya Pakistan hii leo imekamilisha maandalizi ya uchaguzi wa bunge ambao rais Musharraf ameahidi utafanyika kabla Januari 9 mwakani. Vyama vya upinzani vimetishia kuugombea uchaguzi huo vikisema hautakuwa na maana yoyote iwapo utafanyika katika hali ya hatari. Katibu wa tume ya uchaguzi, Kanwar Dilshad, amesema mjini Islamabad kwamba tume hiyo itafanya kila inaloweza kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa njia huru na ya haki.

Huko mjini Lahore polisi wamewatia mbaroni viongozi zaidi wa upinzani, akiwemo mchezaji mashuhuri wa zamani wa mchezo wa cricket, Imran Khan, kwenye mikutano ya hadhara ya kupinga utawala wa hali ya hatari nchini Pakistan. Mamia ya mawakili, waandishi wa habari na wafanyakazi wa upinzani, wamefanya maandamano kadhaa katika maeneo mbalimbali ya Pakistan kwa siku ya 12 kumpinga rais Musharraf na kumshinikiza arejeshe utawala wa kidemokrasia.

Wanafunzi kadhaa wamejiunga na maandamano hayo wakati Imran Khan alipowasili katika chuo kikuu cha Punjab mashariki mwa Lahore. Lakini polisi ambao walikuwa wamevaa mavazi ya kiraia, walimkamata na kumpeleka kwenye jengo moja katika chuo kikuu hicho. Saa chache baadaye wakampeleka kwenye kituo cha polisi.

Imran Khan amekuwa mafichoni tangu hali ya hatari ilipotangazwa mnamo Novemba 3 na amekuwa akiwatolea mwito wanafunzi wafanye maandamano ya kuupinga utawala wa kiimla wa rais Pervez Musharraf. Jaji wa zamani wa mahakama kuu ya Pakistan, Wajihuddin Ahmad, ana matumaini makubwa ufanisi utapatikana nchini Pakistan.

´Nina matumaini makubwa. Nahisi Wapakistan wameamka baada ya muda mrefu. Hatuamini migomo, hatuamini maandamano. Tunaamini msimamo wa kanuni na nadhani tutafanikiwa.´

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan aliye uhamishoni, Nawaz Sharrif, amesema leo kwamba yuko tayari kushirikiana na kiongozi wa upinzani, Benazir Bhutto, kupinga utawala wa kijeshi wa rais Musharraf. Benazir Bhutto amekuwa akijaribu kuunda muungano wa upinzani na amekuwa akizungumza na wanachama wa chama cha Nawaz Sharif.

 • Tarehe 14.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH6t
 • Tarehe 14.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH6t

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com