1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mtu wa kwanza kufika mwezini, afariki dunia

Mtu wa kwanza kufika mwezini, mwanaanga wa kimarekani Neil Armstrong amefariki akiwa na umri wa miaka 82. Rais Barack Obama ametoa rambirambi zake, na kusema mwanaanga huyo ni miongoni mwa mashujaa wakubwa wa Marekani.

Mwanaanga Neil Armstrong

Mwanaanga Neil Armstrong

Katika tangazo lililotolewa na familia ya Armstrong kufuatia kifo chake, mwanasayansi huyo ametajwa kuwa shujaa wa Marekani, ambaye muda wote yeye alisisitiza kuwa alichokifanya kilikuwa wajibu wake kikazi. Familia yake imesema kuwa kifo chake kimetokana na matatizo yaliyofuatia upasuaji wa moyo.

Neil Armstrong alitua mwezini tarehe 20 Julai, 1969, akiwa katika chombo kilichoitwa Apollo na kusema ''hiyo ilikuwa hatua ndogo ya binadamu, lakini mapinduzi makubwa kwa ubinadamu''.

Picha za Armstrong akitembea mwezini zilionyeshwa moj kwa moja kwenye televisheni

Picha za Armstrong akitembea mwezini zilionyeshwa moj kwa moja kwenye televisheni

Rais Obama atoa rambirambi

Rais wa Marekani Barack Obama amesesema Neil Armastrong atabakia kuwa miongoni mwa mashujaa mashuhuri wa Marekani, si kwa wakati wake tu, bali milele. Amesema Armstrong pamoja na wenzake 11 katika chombo cha Apollo, walibeba matarajio ya taifa zima la Marekani katika safari yao ya anga mwaka 1969.

''Waliionyesha dunia ari ya Marekani kuangalia mbali zaidi ya yale yanayofikirika, na kuthibitisha kuwa penye juhudi na maarifa, kila kitu kinawezekana'' alisema rais Obama, na kuongeza kuwa ujumbe alioutoa Armstrong baada ya kukanyaga kwenye ardhi ya mwezini, ni mafanikio ya binadamu ambayo kamwe hayatasahaulika.

Mfano wa kuigwa

Kulingana na wasifu wa Armstrong ambao umechapishwa na shirika la anga la Marekani, NASA, mwanaanga huyo aliyezaliwa jimboni Ohio mwaka 1930, alisafiri kwa ndege kwa mara ya kwanza akiwa na miak sita, na kupata leseni ya kuendesha ndege akiwa na miaka 16, hata kabla ya kujua kuendesha gari.

Alitumikia jeshi la Marekani kama rubani wa ndege za kivita wakati wa vita vya Korea, na baadaye akajiunga na masomo ya sayansi ya anga. Baadaye aliajiriwa kama rubani wa kuzifanyia ndege majaribio. Neil Armstrong alijiunga na programu ya anga mwaka 1962, na kurusha chombo cha kwanza cha anga miaka minne baadaye. Aliteuliwa kuwa kiongozi wa wanaanga walioshiriki katika safari ya Apollo, ambayo iliwafikisha wanadamu wa kwanza mwezini. Hatua yake ya kwanza mwezini iliangaliwa na mamilioni ya watu duniani kwa njia ya televisheni.

Mkuu wa Shirika la Anga la Marekani, NASA, Charles Bolden ametuima salamu zake za rambirambi kwa familia ya Armstrong. Charles Bolden amesema wakati wowote kutakapokuwa na vitabu vya historia, jina la Neil Armstrong litaandikwa kwenye kurasa za vitabu hivyo. Amesifia jinsi Neil Armstrong alivyoishi maisha ya unyenyekevu, na kusema kuwa mfano wake ni wa kuigwa.

Shauku ya ujana wake waikupotea

Familia ya Armstrong imesema kuwa mwanaanga huyo aliendelea kufuatilia maendeleo ya safari za anga, na kila alipofanya hivyo shauku yake ya ujana ilijitokeza tena.

Neil Armstrong alistaafu kutoka NASA mwaka 1971na alifanya kazi kwenye bodi ya wakurugenzi. Hakupenda kuwa mtu wa kujionyeshaonyesha, isipokuwa mara chache tu kwenye kumbukumbu za safari ya kwanza mwezini, au akitoa akiunga mkono kuendelea kwa utafiti wa anga.

Familia yake imesema kuwa ingawa Neil Armstrong alipenda kuishi maisha yake bila bugudha, alifurahia ujumbe wenye nia njema kutoka kote ulimwenguni.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPA

Mhariri: Sudi Mnette

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com