Mshindi wa Ballon d'Or kujulikana Jumatatu
3 Desemba 2018Mshindi wa kiatu cha dhahabu Ballon d'Or mwaka 2018 atapatikana katika sherhe itakayofanyika mjini Paris leo Jumatatu usiku, ambapo Luka Modric wa Croatia pamoja na wachezaji kadhaa wa kikosi kilichoibuka mshindi katika kombe la dunia cha Ufaransa wakitaraji hatimaye kufikisha mwisho miaka 10 ya ushindi wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.
Wachezaji sita wa kikosi cha Ufaransa ni miongoni mwa wachezaji 30 walioteuliwa kwa ajili ya tuzo hiyo ambayo inatayarishwa na jarida la michezo la Ufaransa na kupigiwa kura na waandishi habari 180 duniani kote. Miongoni mwao ni pamoja na Kylian Mbappe, Antoine Griezmann , Raphael Varane, Hugo Lloris, Paul Pogba na N'Golo Kante.
Na kwa upande wa shirikisho la kandanda barani Ulaya, limeidhinisha kuundwa kwa mashindano ya tatu ya UEFA ya vilabu jana Jumapili, mashindano ambayo yatakuwa katika mfumo kama Champions League ya sasa pamoja na Ligi ya Ulaya, Europa League kuanzia mwaka 2021.
Katika mkutano wao mjini Dublin , kamati kuu ya UEFA ilikamilisha mipango ya kuanzisha mashindano hayo, kwa jina la UEL2 na yatahusisha timu 32 katika awamu ya makundi , katika msimu wa 2021 hadi 2024.
Katika bara la Afrika , klabu ya Morocco ya Raja Casablanca imefikisha mwisho miaka 15 ya kusubiri kunyakua taji la bara la Afrika kwa kushinda kombe la CAF la shirikisho katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo jana Jumapili licha ya kufungwa mabao 3-1 katika mkondo wa pili wa fainali dhidi ya V Club ya Congo. Raja ambayo ilishinda mara ya mwisho kombe hilo mwaka 2003, iliishinda V Club kwa mabao 3-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza mjini Casablanca Jumapili iliyopita na kufanikiwa kulinyakua kombe hilo kwa jumla ya mabao 4-3 katika michuano ya mikondo miwili ya fainali.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre / ape
Mhariri: Mohammed Khelef