1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiRwanda

Bunge la Uingereza laidhinisha kupelekwa wahamiaji Rwanda

23 Aprili 2024

Mpango wenye utata wa serikali ya Uingereza wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda hatimaye umeidhinishwa na Bunge mapema siku ya Jumanne.

https://p.dw.com/p/4f4UE
London | Mpango wa Uingereza kuwapeleka wahamiaji Rwanda waidhinishwa
Matokeo ya kura kuhusu mswada wa kuwapeleka nchini Rwanda waomba hifadhi wanaowasili Uingereza yakisomwa Bungeni:22.04.2024Picha: House of Commons/UK Parliament/PA Wire/empics/picture alliance

Hatua hiyo imefikiwa baada ya vuta ni kuvute iliodumu hadi usiku wa manane kati ya baraza la juu la bunge la Uingereza - House of Lords na baraza la House of Commons.   

Wajumbe wa baraza hilo la juu, ambao hutathmini sheria iliyopendekezwa, walirejesha mara kadhaa mswada huo kwa marekebisho katika chumba cha chini lakini hatimaye waliafiki kuwa mswada huo hauhitaji mabadiliko zaidi, na hivyo kuhakikisha kuwa mswada huo sasa utakuwa sheria.

Uingereza | Waziri Mkuu Rishi Sunak
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak akiahidi kutekeleza mpango huoPicha: Toby Melville/AP Photo/picture alliance

Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak aliahidi kuanza mnamo miezi michache ijayo, kuwapeleka nchini Rwanda waomba hifadhi wanaowasili nchini humo, kama mpango wenye utata wa serikali ya Uingereza wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda.

Kuwapeleka wahamiaji Rwanda, ni sehemu muhimu ya majibu ya Waziri Mkuu Sunak katika kukomesha vitendo vya waomba hifadhi kuingia  kinyume cha sheria nchini Uingereza.

Mpango wa kukabiliana na idadi ya wahamiaji wanaowasili Uingereza

Wahamiaji wanaojaribu kuingia Uingereza
Wahamiaji hao huhatarisha maisha kwa kutumia usafiri wa boti ndogo wakitokea UfaransaPicha: Gareth Fuller/empics/picture alliance

Wahamiaji hao huhatarisha maisha kwa kutumia usafiri wa boti ndogo wakitokea Ufaransa. Pendekezo la kuwaondoa wahamiaji Uingereza limekabiliwa na utata na changamoto za kisheria tangu aliyekuwa Waziri Mkuu Boris Johnson alipoliwasilisha mwaka 2022.

Idadi ya wahamiaji waliowasili Uingereza kwa boti ndogo iliongezeka hadi kufikia 45,774 mnamo mwaka 2022 kutoka 299 miaka minne iliyopita. Wahamiaji hao huwalipa magenge ya wahalifu maelfu dola ili kuwavusha kwa boti hizo hadi Uingereza.

Soma pia: Mpango wa Uingereza kuwahamishia wakimbizi Rwanda kugharimu pauni milioni 300

Mwaka jana, idadi ya waliowasili kwa boti ndogo nchini humo ilipungua hadi 29,437 wakati serikali mjini London ikipambana vikali na makundi hayo ya wahalifu na kufikia makubaliano ya kuwarejesha Waalbania katika nchi yao.

Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Kamati ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa iliitolewa wito Uingereza kuachana na mpango huo wenye utata wa kuwapeleka waomba hifadhi nchini Rwanda, kwa hoja kwamba makubaliano kati ya nchi hizo mbili hayakujali uamuzi wa Mahakama Kuu ya Uingereza iliyosema kuwa  mpango huo unakinzana na sheria za kimataifa.

(Chanzo: AP)