1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mpango wa kulichoma Bunge la Misri wagundulika

Baraza la kijeshi la utawala nchini Misri lililochukua madaraka wakati rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak alipotolewa madarakani Februari mwaka huu, limesema limegundua mpango ulionuiwa kulichoma jengo la bunge nchini humo.

Bunge la Misri

Bunge la Misri

Jenerali Adel Emara mwanachama wa baraza kuu la jeshi nchini humo amesema amepokea simu na kuarifiwa kuhusu njama ya kuchoma jengo la bunge na kuwa kuna makundi ya waandamanaji katika uwanja wa Tahrir walio tayari kutekeleza hilo.

Mwandishi wa shirika la habari la AFP aliyeko katika uwanja wa Tahrir, amesema mamia ya waandamanaji wengine walikuwa katika uwanja huo wakihudhuria mazishi ya mmoja wao aliyeuwawa katika ghasia zinazoendelea. Mbali kidogo na uwanja huo katika jengo la kihistoria ambapo stakabadhi muhimu za taifa hilo zilichomeka waandamanaji wamekuwa wakijaribu kuokoa angalau baadahi ya stakabadhi hizo.

Hata hivyo taarifa ya jenerali Emara imetolewa wakati ambapo mtu mwengine mmoja ameuwawa katika mapigano kati ya waandamanaji na majeshi na kuchangia katika ongezeko ya mauaji kufikia 11 tangu kuanza kwa mapambanao hayo siku nne zilizopita. Mamia wengine wamejeruhiwa vibaya.

Ghasia hizo ziliigubika shughuli nzima ya kuhesabu kura katika uchaguzi wa ubunge uliomalizika, unaoonesha chama cha kiislamau kikichukua uongozi na pia kuzua hisia tofauti kutoka jamii ya kimataifa ikiwemo umoja wa mataifa pamoja na Marekani.

Huku hayo yakiarifiwa majeshi ya usalama yanayopambana na wapinzani wa jeshi linalotawala mjini Cairo yamezua hisia mbali mbali huku Marekani ikiwa na wasiwasi mkubwa juu ya mapigano hayo na kuhimiza haki za binadamu kuheshimiwa.

Polisi na majeshi wanaotumia marungu na vitoa machozi walionekana wakiwakimbiza waandamanaji nje ya uwanja wa Tahrir, huku waandamanaji hao wakionekana kurusha mawe.

Ban Ki-Moon

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Ban Ki Moon, amelaani vikali utumiaji wa nguvu dhidi ya waandamanaji, hatua iliyogubika shughuli nzima ya uchaguzi wa kwanza huru nchini humo. Hillary Clinton, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, amehimiza majeshi ya usalama kuheshimu na kulinda haki ya raia wote nchini Misri. Clinton pia amewataka waandamanaji kujiepusha na visa vitakavyochochea ghasia zaidi.

Shirika moja la habari la MENA Misri limeripoti kiongozi wa mashtaka nchini humo amewatia nguvuni watu 123 wanaotuhumiwa kwa makosa ya kuwarushia mawe polisi na majeshi na kuchoma moto kwa baadhi ya majengo ya serikali. Tayari watu 53 wameachiwa huru.

Ghasia hizi zimewakasirisha Wamisri wengi wanaotaka kumalizika haraka kwa wimbi la mageuzi lililoanza mapema mwaka huu na sasa kuyumbisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa Misri.

Mwandishi: Amina Abubakar AFPEE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com