1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOSUL : Watu 175 wauwawa kwa miripuko Iraq

15 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBZ3

Nchini Iraq takriban watu 175 wameuwawa na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa katika mirupuko ya kujitolea muhanga maisha kwa kutumia malori manne yaliotegwa mabomu.

Repoti zinasema kwamba shambulio hilo lililoratibiwa dhidi ya jamii ya Wayazidi wa kabila la watu wachache la Wakurdi karibu na Mosul kaskazini mwa Iraq ni mojawapo ya shambulio baya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika vita vya miaka minne nchini humo.Vyombo vya habari vya Iraq vimesema kwamba malori mawili kati ya hayo yaliosheheni mabomu yameripuliwa kwa pamoja katika eneo la maakazi ya Siba Sheikh Khidr na baadae kufuatiwa na shambulio la mizinga.

Generali David Petraeus mkuu wa vikosi vya muungano nchini Iraq anasema operesheni mpya ilioanza inayojulikana kama Shambulio la Phantom dhidi ya waasi ni ngumu lakini sio kwamba haina matumaini na kwamba kwa kushirikiana na washirika wao wa Iraq wanaweza na lazima wataibuka washindi.

Generali huyo wa Marekani anatarajiwa kutowa repoti muhimu juu ya maendeleo ya operesheni za kijeshi nchini Iraq mapema mwezi wa Septemba.

Wakati huo huo naibu waziri wa mafuta nchini Iraq ametekwa nyara na waasi na wanajeshi watano wa Marekani wamekufa baada ya helikopta yao kuanguka wakati wa majaribio ya safari.