1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MORONI:Mohamed Bacar ajitangaza mshindi

11 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBsf

Kiongozi wa zamani wa kisiwa cha Nzouani cha Komoro Mohamed Bacar amejitangazia ushindi katika uchaguzi aliolazimisha mwishoni mwa juma lililopita.Umoja wa Afrika AU na serikali kuu ya Komoro iliahirisha uchaguzi huo hadi tarehe 17 mwezi wa Juni.Kiongozi huyo wa Nzouani wa zamani ataapishwa jumatano ijayo na kuunda serikali yake siku inayofuata kwa mujibu wa Abdou Madi mmoja wa washauri wake waliozungumza na shirika la habari la Reuters.

Uchaguzi huo wa jumapili iliyopita ulifanyika huku kukiwa na hali ya wasiwasi visiwani Komoro ambako wanajeshi wa Bwana Bakari waliwaua askari wawili wa shirikisho mwezi uliopita.Polisi waliwauwa watu wengine watatu wiki jana.Serikali kuu ya Komoro iliahirisha uchaguzi huo kwa wiki moja kwasababu za kiusalama lakini uchaguzi ukafanyika kwa lazima.

Kulingana na maafisa wa serikali waangalizi wa kimataifa kutoka Umoja wa Afrika AU na makundi mengine waliondolewa kisiwani humo kabla uchaguzi kufanyika.Komoro ina visiwa vitatu Nzouani,Moheli na Ngazija vilivyo na uhuru wa kujiongoiza na vinapokezana uongozi wa serikali kuu kama ilivyokubaliwa mwaka 2001.