1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Mapigano yaingia siku ya tano

22 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC85

Mashambulizi mazito ya mizinga yameutingisha mji mkuu wa Mogadishu leo hii na kuzusha hofu ya kuwepo kwa maafa zaidi ya kiraia wakati mapigano kati ya vikosi vya Ethiopia na waasi wa Kiislam yakiingia siku yake ya tano nchini Somalia.

Vikosi hivyo hasimu vimekuwa vikishambuliana kwa mizinga mizito baada ya vita vya hapa na pale wakati wa usiku kuharibu majengo kaskazini na kusini mwa Mogadishu.Idadi ya maafa kutokana na mapigano hayo haikuweza kufahamika mara moja.

Kwa mujibu wa shahidi mmoja katika eneo la Gupta kusini mwa Mogadishu vifaru vya Ethiopia vimekuwa vikishambulia ovyo kwa mizinga na makombora kuelekea maeneo ya kiraia na kwamba makombora hayo yamekuwa yakituwa kila mahala.

Mapigano hayo yaliozuka hapo Jumaatano yamegharimu maisha ya takriban raia 168 na kujeruhi wengine mamia.Wakaazi wanasema idadi hiyo inaweza hata kuwa kubwa zaidi kwa vile maeneo mengi ya mapigano hayawezi kufikiwa.

Imeelezwa kwamba pande zote mbili zinatumia bunduku za rashasha na mizinga ya kutungulia ndege.