1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Mapambano yapamba moto

22 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CChN

Kiongozi wa Muungano wa Mahkama za Kiislam nchini Somalia ameyaita mapigano karibu na makao makuu ya serikali ya mpito huko Baidoa kuwa ni vita kamili na kuilaumu nchi jirani ya Ethiopia kwa kuanzisha mapigano hayo.

Mapigano makali kati ya Vikosi vya serikali vikiungwa mkono na Ethiopia na wapiganaji wa Kiislam yamekuwa yakiendelea hapo jana kwa siku ya pili mfululizo kwa kuingizwa vitani kwa vifaru vya Ethiopia huku pande zote mbili zikidai kusababisha maafa makubwa kwa mwenzake na ikiwa ni siku moja baada ya kukutana na mjumbe wa Umoja wa Ulaya Louis Michel na kuwashawishi kurudi kwenye mazungumzo ya amani bila ya masharti.

Mamia ya wanajeshi wa Ethiopia inasemekana kuwa wako nchini Somalia kuwafunza wanajeshi wa serikali lakini uongozi wa Kiislam unadai kwamba wanajeshi hao wa Ethiopia wako nchini Somalia kwa maelfu wakipambana bega kwa bega na wanajeshi wa serikali.

Mapema Mkuu wa Muungano wa Mahkama za Kiislam Sheikh Hassan Dahir Aweys amewataka wananchi wa Somalia kuingia vitani kupambana na wanajeshi wa Ethiopia baada ya kumalizika kwa siku mbili muda iliowapa waondoke nchini humo vengienvyo iwe tayari kwa vita.