1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mlipuko mwingine watokea kaskazini mwa Kenya

27 Oktoba 2011

Nchini Kenya mripuko mwengine umetokea kaskazini mwa nchi hiyo ambapo watu wanane wamekufa, baada ya basi moja kulipuliwa.

https://p.dw.com/p/1304e
Shambulio lingine limetokea eneo la Mandera

Tukio hilo ni la tatu kutokea, wiki hii ambapo kundi la al shaabab nchini Somalia linahusishwa, kufuatia kitisho ilichotoa kuishambulia Kenya kupinga hatua ya nchi hiyo kutuma majeshi yake nchini Somalia. Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani DPA, shambulio hilo limetokea katika eneo la Mandera kiasi cha kilomita elfu moja kaskazini mwa jiji la Nairobi.

Lakini kwa mujibu wa mtandao wa kituo cha radio cha jijini humo Capital FM ni kwamba watu waliokufa katika shambulio hilo ni wanne. Kimesema kuwa basi lililokuwa limewabeba watu wanane wakiwemo wasimamizi wa mitihani pamoja na maafisa wa polisi waliokuwa wakisindikiza mitihani ya kidato cha nne nchini humo lilishambuliwa na kombora ambapo wanne kati yao inaarifiwa kuwa wamekufa. Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa hizo ni kwamba idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka.

Mashambulizi mawili ya maguruneti yalitokea jijini Nairobi mwanzoni mwa wiki hii ambapo mtu mmoja alikufa na wengine 22 kujeruhiwa. Mtu mmoja amekiri mahakamani kuhusika na mashambulizi hayo ya Nairobi, hiyo ikiwa ni baada ya polisi kukamata silaha kadhaa katika nyumba moja jijini humo. Mtu huyo Elgiva Bwire Oliacha alisema kuwa alifanya hivyo akiwaunga mkono al Shaabab.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia, Abdiweli Mohamed Ali, amesema kuwa anaunga mkono hatua ya jeshi la Kenya kuingia nchini Soamlia kuwasaka waasi wa al Shaabab.

Kauli hiyo inakuja siku moja baada ya Rais wa serikali hiyo ya Somalia Sheikh Sharrif Ahmed kusema kuwa anapinga hatua ya jeshi hilo kuingia nchini Somalia kinyume na makubaliano ya awali.

Amesema kuwa anaunga mkono harakati za jeshi la Kenya nchini Somalia akisema kuwa kuwepo kwa jeshi hilo, wananufaika na mafunzo, pamoja na misaada mingine inayotolewa kwa vikosi vya serikali hiyo ya mpito.

Akizungumza katika mahojiano na shirika la habari la Uingereza Reuters, waziri huyo mkuu wa Somalia hata hivyo amesema kuwa pamoja na kuunga mkono kuwepo kwa vikosi vya Kenya nchini Somalia, lakini jeshi la serikali hiyo ndiyo lisimamie kikamilifu oparesheni hiyo na siyo jeshi la Kenya.

Amesema Kenya ina haki ya kuwasaka wanamgambo wa al Shaabab ndani ya Somalia na kuwaangamiza, kutokana na madhara yanayosababishwa na wanamgambo hao nchini Kenya.

Akizungumzia juu ya hatua hiyo ya jeshi la Kenya Kamishna wa Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra amesema.

"Kama unavyofahamu tunashirikiana kwa karibu zaidi na mataifa ya IGAD, nchi jirani pamoja na washirika wengine, na njia yoyote ile ya kuwadhoofisha al Shaabab ni lazima iwe ndani ya jukumu zima linaloungwa mkono nasi sote"

Jeshi la Kenya lilingia nchini Somalia siku 12 zilizopita kupambana na wanamgambo wa al Shaaba ambao wanatuhumiwa kwa vitendo vya utekaji nyara raia wa kigeni nchini Kenya. Hata hivyo Rais wa Somalia hapo jana alisema kuwa hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa kati ya serikali yake na Kenya kutuma majeshi yake nchini humo, lakini akasema waziri wake mkuu, Abdiweli Mohamed Ali, atakuwa kiungo kati ya serikali yake na Kenya.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/DPA/Capital FM/ZPR

Mhariri:Josephat Charo