1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Tokyo kuamua mustakabali wa Afghanistan

Admin.WagnerD6 Julai 2012

Mkutano wa kimataifa kuhusu Afghanistan unaanza Jumapili mjini Tokyo, Japan, ambapo rais Hamid Karzai, ataomba dola bilioni 4 kutoka kwa wafadhili. Lakini atalaazimika kujibu maswali magumu kuhusu rushwa.

https://p.dw.com/p/15T95
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.Picha: picture-alliance/dpa

Mkutano huo unalenga kuhamasisha misaada zaidi kwa nchi hiyo, ili kuimarisha ulinzi na usalama pindi majeshi ya kigeni yatakapoondoka nchini humo, mwishoni mwa mwaka 2014.

Wawakilishi kutoka mataifa 70 na mashirika ya kimataifa wataweka mikakati ya kuhakikisha uwajibikaji, kuhakikisha Afghanistan inafanya kazi ya ziada kuboresha utawala na usimamizi wa fedha, na kulinda mchakato wa kidemokrasia, utawala wa sheria na haki za binaadamu, hususani za wanawake.

Msaada kutoka nje tangu uvamizi wa Marekani mwaka 2001 umesaidia kuboresha elimu na afya, ambapo karibu watoto milioni 8, wakiwemo wasichana milioni 3 wamesailiwa mashuleni. Hii inalinganishwa na watoto milioni moja tu waliokuwa wanapata elimu muongo mmoja uliyopita, ambapo watoto wa kike walizuiwa kwenda shule na watawala wa Taliban.

Wanajeshi wa Ujerumani walioko nchini Afghanistan
Wanajeshi wa Ujerumani walioko nchini AfghanistanPicha: AP

Kuboreshwa kwa miundombinu ya afya kumepunguza vifo vya watoto kwa nusu na kupanua upatikanaji wa huduma zake kufikia karibu asilimia 60 ya raia wa Afghanistan, ambao ni zaidi ya milioni 25, ikilinganishwa na asilimia 10 waliyokuwa wanafikiwa na huduma za afya mwaka 2001.

Changamoto za rushwa na ubadhirifu mwingine
Lakini wasiwasi umekuwa ukiongezeka miongoni mwa wafadhili kuhusiana na rushwa iliyokithiri nchini humo, na kusababisha wengine kushindwa hata kutimiza ahadi zao za misaada. Maafisa kadhaa wa ngazi za juu wamechunguzwa kuhusiana na tuhuma za rushwa, lakini hawajawahi kupelekwa mbele ya sheria. Kibaya zaidi, tuhuma nyingine za rushwa zimekuwa zikimhusisha kwa karibu hata Rais Hamid Karzai.

Karzai atakabiliwa na wakati mgumu, kuishawishi jumuiya ya kimataifa iliyochoshwa na vita na kushindwa kwake kupambana na rushwa, zaidi ya muongo mmoja tangu kuondolewa madarakani kwa utawala wa Taliban. Afghanistan imeshapokea zaidi ya dola bilioni 60 za msaada kama huo tangu mwaka 2002. Benki y Dunia inasema msaada kutoka nje unachangia karibu sawa na jumla ya pato la ndani la nchi hiyo.

Ufadhili huo, ambao ni muhimu kuwezesha utoaji wa huduma za kijamii kama elimu, afya na miundombinu, unatarajiwa kupungua kwa kiasi kikubwa baada ya kuondoka kwa vikosi ya kimataifa, licha ya ukweli kwamba nchi hiyo bado inakabiliwa na kitisho kutoka kwa Wataliban na makundi mengine ya wanamgambo.

Magari yaliobeba shehena ya vikosi vya NATO yakiingia nchini Afgnanistan baada ya Pakistan kufungua njia ilizozifunga kwa miezi saba.
Magari yaliobeba shehena ya vikosi vya NATO yakiingia nchini Afgnanistan baada ya Pakistan kufungua njia ilizozifunga kwa miezi saba.Picha: DW

Karzai ataka dola bilioni 4 kila mwaka
Rais Karazai amesema ataomba dola bilioni 4 kila mwaka kwa miaka mitatu ya kwanza, ya kile serikali yake ilichokiita kipindi cha mageuzi kuanzia mwaka 2015 hadi 2025. Kiasi hiki ni juu ya kile cha dola bilioni 4.1, zilizoahidiwa wakati wa Mkutano wa Jumuiya ya Kujihami, NATO uliofanyika Chicago nchini Marekani, kama ufadhili kwa vikosi vya ulinzi na usalama kuanzia mwaka 2015 hadi 2017.

Benki ya Dunia imesema Afghanistan itahitaji kati ya dola bilioni 3.3 hadi biliono 3.9 za matumizi yasiyo ya kijeshi kila mwaka kwa kipindi hicho cha miaka mitatu ya mpito, ili kufidia nakisi ya pato lake la ndani, ambalo ni zaidi ya dola bilioni 17. Afghanistan iliorodheshwa mwaka jana kama nchi ya tatu duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha rushwa.

Shule ya kisasa iliyoko mjini Kabul. Misaada ya kimataifa imesaidia kuboresha elimu nchini Afghanistan.
Shule ya kisasa iliyoko mjini Kabul. Misaada ya kimataifa imesaidia kuboresha elimu nchini Afghanistan.Picha: DW

Uingereza iko tayari kuendelea kusaidia, lakini Marekani yapunguza msaada
Licha ya wasiwasi huo, Uingereza na washirika wengine wanakubaliana kwamba Afghanistan itahitaji kusaidiwa baada ya mwaka 2014, ili isirudi tena katika vurugu na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Tayari Uingereza imeahidi kutoa dola bilioni 280 katika msaada wa maendeleo hadi kufikia mwaka 2017.

Uchumi wa Afghanistan ambao unategemea zaidi misaada ya kimataifa na matumizi ya kijeshi, unatizamiwa kushuka baada ya mwaka 2014. Tayari Marekani imepunguza kwa nusu, msaada wa dola bilioni 4 iliyoutoa mwaka 2010 na inatarajia kuupunguza zaidi mwaka ujao.

Benki ya Dunia imeonya kuwa kupunguza msaada kwa nchi hiyo, kunaweza kusababisha kuanguka kama kule kulikoshuhudiwa baada ya kuondoka kwa Wasovieti mwaka 1989. Mashirika ya Kibinaadamu yanahofu kwamba Mkutano wa Tokyo unaweza kujikita zaidi katika uwajibikaji na matumizi ya misaada inayozidi kupungua na kuwasahau raia wa nchi hiyo ambao ni wahitaji.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akibadilisha hati na rais Hamid Karzai, baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano, Mei 16 mwaka huu.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akibadilisha hati na rais Hamid Karzai, baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano, Mei 16 mwaka huu.Picha: Reuters

Afghanistan laazima ifanye ushawishi wa kuridhisha
Japan inakiri kwamba Mkutano hautakuwa wa kutoa tu ahadi za misaada. Tadamichi Yamamoto, mwakilishi maalumu wa Afghanistan na Pakistan katika wizara ya mambo ya nje ya Japan, alisisitiza kuwa Afghanistan laazima ionyesha kuwa inaweza kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo.

Ahadi hiyo inatarajiwa kuwasilishwa katika anadiko ambalo litaabainisha masharti kadhaa, ikiwemo uchaguzi huru na wa haki mwaka 2014, maboresho katika usimamizi wa fedha, kuheshimu haki za binaadamu na utawala wa sheria.

Misaada hii itatolewa kupitia bajeti ya serikali au mifuko inayodhibitiwa na mashirika ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia. Ili kuwashawishi wafadhili wakubali kutoa misaada hiyo, serikali ya Afghanistan imetengeneza miswada 22 ya vipaumbele vya maendeleo yenye vipengele vikali vya utekelezaji na uwajibikaji.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE
Mhariri: Mohamed Khelef