1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Paris kukusanya fedha za mazingira

Oumilkheir Hamidou
12 Desemba 2017

Viongozi wa dunia wanakutana mjini Paris kusaka njia za kukusanya fedha kugharimia juhudi za kupambana na kuzidi hali ya ujoto duniani, miaka miwili baada ya kufukiwa makubaliano jumla ya Paris

https://p.dw.com/p/2pE6a
Frankreich One Planet Summit in Paris Austragungsort
Picha: Getty Images/AFP/L. Marin

 

Bila ya kukusanywa dola trilioni kadhaa za kimarekani  ili kuwekezwa katika teknolojia ya nishati safi, malengo yaliyowekwa katika makubaliano ya Paris ya kupunguza kiwango cha joto kiwe chini ya nyuzi joto mbili Celsius yatasalia kuwa ndoto. Wanaonya washiriki wa mkutano huo wa Paris.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anakutana na viongozi wasiopungua 60 wa dunia, ili kujibu tangazo la rais wa Marekani Donald Trump alilolitoa mwezi juni uliopita, kwamba ataitoa Marekani katika makubaliano ya Paris yaliyofikiwa na mataifa karibu 200 baada ya takriban miongo miwili ya majadiliano.

Donald Trump aliyeyataja makubaliano ya Paris kuwa ni "Dhihaka", amezuwia mabilioni ya dola fedha zilizokuwa zimelengwa kugharamia miradi ya kupunguza mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na dala bilioni mbili toka dala bilioni tatu, ambazo Marekani chini ya utawala wa mtangulizi wake Barack Obama iliahidi kwaajili ya fuko la mazingira ya kijani.

Rais Trump akiwakaribisha mwenyekiti wa benki kuu ya dunia Jim Yong Kim na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres
Rais Trump akiwakaribisha mwenyekiti wa benki kuu ya dunia Jim Yong Kim na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio GuterresPicha: Getty Images/AFP/P. Wojazer

Emmanuel Macron ameitolea wito jumuia ya kimataifa izidi kujizatiti kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Tuko mbali sana kuyafikia malengo ya maakubaliano ya Paris" ameliambia gazeti la le Monde.

Mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya mazingira, Patricia Espinosa ameonya "hatua za kisiasa hazitotosha ikiwa fedha za kutosha hazitopatikana kuhakikisha juhudi za kupunguza moshi wa sumu unaotoka viwandani ni imara na za kudumu.

Ingawa shujaa miongoni mwa wanaopigania usafi wa mazingira, rais wa zamani wa Marekani Barack Obama hahudhurii mkutano wa Paris, hata hivyo wenye viwanda kadhaa wa Marekani, wawakilishi wa serikali za majimbo na viongozi wa serikali za majimbo wanahudhuria mkutano huo ikiwa ni pamoja na meya wa zamani wa New-York Michael Bloomberg, gavana wa zamani wa California Arnold Schwarzenegger na mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates.

Meya wa zamani wa jimbo la Marekani la California, Arnold Schwatzenegger akiwasili Elysée mjini Paris
Meya wa zamani wa jimbo la Marekani la California, Arnold Schwatzenegger akiwasili Elysée mjini ParisPicha: Getty Images/AFP/C. Archambault

Wamarekani wanawajibika mbele ya makubaliano ya Paris licha ya tangazo la rais Trump

Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje  John Kerry anasema:"Mameya 90 wa Marekani wameahidi kutekeleza makubaliano ya Paris. Na nna kukuhakikishieni katika wakati ambapo Donald Trump anataka kuitoa Marekani katika makubaliano hayo,wamarekani hawataki kutoka.Tunaendelea kuwajibika na makubaliano ya Paris. Na hilo ni muhimu kwa watu kulijua."Amesema hayo waaziri wa zamanin wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, John Kerry

Nje ya jengo la mkutano, waandamanaji wanapaza sauti kuitaka Ufaransa iache kulipia nishati inayotokana na mafuta, gesi na makaa ya mawe.

Nishati hiyo inalaumiwa kuwa chanzo cha kuchafuliwa mazingira na kusababisha kuongezeka hali ya ujoto duniani.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman