1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa NAM wamalizika Tehran

Mkutano wa mataifa yasiyofungamana na upande wowote NAM, umemalizika mjini Tehrani, Irani Ijumaa jioni(31.08.2012) huku rais Ahmednejad akiahidi amani kwa dunia.

Baadhí ya washiriki wa mkutano wa mataifa yasiyofungamana na upande wowote.

Baadhí ya washiriki wa mkutano wa mataifa yasiyofungamana na upande wowote.

Mkutano huo ulimalizika baada ya siku mbili za majadiliano ambayo wakati mwingine yalikuwa yakipamba moto juu ya mpango wa kinyuklia wa Iran na mgogoro wa Syria, mambo ambayo yalifunika juhudi za Iran kutaka kuungwa mkono dhidi ya mataifa ya magharibi. Pamoja na hayo, wawakilishi kutoka mataifa 120 wanachama wa mkutano huo walikubaliana juu ya tamko lililolaani vikwazo, na kuunga mkono haki ya Iran na mataifa mengine kuwa na nishati ya nyuklia kwa matumizi salama. Pia waliunga mkono kuundwa kwa taifa la Palestina.

Baadhí ya washiriki wa mkutano wa mataifa yasiyofungamana na upande wowote.

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadnejad akisalimiana na waziri mkuu wa Iraq Nour Al-Maliki wakati wa mkutano huo.

Rais Mahmoud Ahmadnejad alisema ujumbe muhimu wa kisiasa kutoka NAM kwenda kwa jumuiya ya kimataifa, ni ujumbe wa urafiki na amani na utayari wake kushughulikia changamoto zinazoikabili dunia."Mataifa wanachama wa NAM walikubaliana juu ya kuwepo uendeshaji mpya wa dunia kwa misingi ya uhuru, haki na urafiki, wote tukiwa na lengo kuu moja la kupata amani enedlevu duniani," alisema Ahmadnejadi ambaye alikuw amwenyekiti wa mkutano huo.

Venezuela mwenyeji wa mkutano wa 17 2015
Waziri wa mambo ya kigeni wa Venezuela Nicolas Maduro alisema muda mfupi baada ya kufungwa kwa mkutano huo kuwa nchini yake ilikuwa imechaguliwa kuwa mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano wa 17 wa mataifa yanaounda vuguvugu la NAM. Maduro alisema mkutano wa 2015 utafanyika katika ulimwengu uliyobadilika, akifafanua kuwa mataifa ya NAM yatakuwa yamepiga hatua katika ujenzi wa ulimwengu mpya usiyo na mataifa ya kibeberu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alitetea uamuzi wake wa kuhudhuria mkutano huo licha ya pingamizi kutoka Marekani, akisema alitumia nafasi hiyo kuishinikiza Iran kuheshimu haki za binaadamu na kuongeza uwazi katika mpango wake wa kinyuklia. "Naamini katika nguvu ya diplomasia na naamini katika majadiliano na naamini katika ushirikiano. Hiki ndicho nilichokifanya wakati wa ziara yangu mjini Tehran," aliliambia shirika la habari la Reuters wakati wa mapumziko mjini Dubai kabla ya kurejea katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akiwa na rais Mahmoud Ahmadinejad mjini Teheran.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akiwa na rais Mahmoud Ahmadinejad mjini Teheran.

Ingawa alikiri kuwa hakuridhishwi na majibu ya viongozi wa Iran aliozungumza nao wiki hii, alikanusha shutuma zilizotolewa na Marekani na Israel kuwa alikuwa anacheza mikononi mwa Iran kwa kukubali kuhudhuria mkutano huo ambao Iran iliutumia kuongeza ushawishi wake wa kidiplomasia. Ban alisema haoni utata wowote katika hatua hiyo kwa kuwa yeye kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ana wajibu wa kushirikiana na mataifa yote wanachama wa umoja huo.

Iran yatumia mkutano kuongeza ushawishi wa kidiplomasia
Iran ambayo imetengwa na majirani zake na inakabiliana na vikwazo vya kimataifa, ilitumia mkutano huo kuonyesha taswira ya nguvu ya diplomasia, kwa watu wake yenyewe na kwa jamii ya kimataifa. Kabla ya mkutano huo, utawala mjini Washington uliweka bayana kuwa ulitaka Ban asihudhurie. Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu naye alimtaka Ban afute mpango wake wa kuhudhuria mkutano huo, akiielezea ziara hiyo kama 'kosa kubwa.'

Mwakilishi wa Iran katika shirika la Umoja wa Mataifa la nguvu za atomiki IAEA Ali Asghar Soltanieh akiwa katika mkutano wa NAM.

Mwakilishi wa Iran katika shirika la Umoja wa Mataifa la nguvu za atomiki IAEA Ali Asghar Soltanieh akiwa katika mkutano wa NAM.

Lakini Ban alitumia nafasi hiyo kuweka wazi kwa utawala mjini Tehrani kuwa vitisho dhidi ya Israel vilikuwa havikubaliki na pia kukanusha kwa Irani kutokea kwa mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudi. Ban aliutumia mkutano huo pia kuyaomba mataifa mengine kuunga mkono juhudi za mpatanishi mpya wa mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi ambaye anaanza kazi rasmi Jumamosi hii (01.09.2012), kama mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu katika mgogoro huo. Ban aliwataka Waziri mkuu wa Syria, Wael al-Halki na waziri wa mambo ya kigeni Walid al-Moualem ambao walihudhuria mkutano huo kuruhusu wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada kupeleka misaada kwa waathirika wa mgogoro huo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, dpae, afpe
Mhariri: Sekione Kitojo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com