Mkutano wa maandalizi wa mawaziri wa nje wa G8 mjini Postdam | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa maandalizi wa mawaziri wa nje wa G8 mjini Postdam

Mawaziri wa nje wa G8 wanapanga kuzungumzia pia mustkbal wa Kosovo watakapokutana baadae hii leo

Bendera za mataifa manane tajiri kwa viwanda na Umoja wa Ulaya

Bendera za mataifa manane tajiri kwa viwanda na Umoja wa Ulaya

Orodha ndefu ya masuala inawasubiri mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa jumuia ya nchi tajiri kwa viwanda G8 watakapokutana hivi punde mjini Postdam nchini Ujerumani.

Hali nchini Irak na mashariki ya kati kwa jumla,mvutano kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran na mustakbal wa Kosovo ni baadhi tuu ya masuala yatakayojadiliwa katika kikako cha maangalizi cha mkutano wa kilele wa G8.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier ambae ndie mwenyekiti wa mkutano huo,amewaalika pia mawaziri wenzake wa kutoka Afghanistan na Pakistan .

Alipokua ziarani hivi karibuni nchini Pakistan na Afghanistan waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier alishuhudia mwenyewe jinsi uhusiano ulivyopooza kati ya nchi hizo mbili.

Serikali ya Afghanistan inawatuhumu majirani zake,hawafanyi vya kutosha katika mapambano dhidi ya wataliban.Wanazidi kukimbilia katika maeneo ya mpakani na Pakistan wanakopatiwa silaha na mafunzo.Hiyo ni sababu kwanini Steinmeier amewaalika mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi zote mbili wahudhurie mkutano wa mawaziri wenzao wa G8 mjini Postdam.Msemaji wa waziri Steinmeier,Jens Plötner anasema mwaliko huo ni katika juhudi za kuhimiza mazungumzo kati ya pande hizo mbili.Bwana Jens Plötner anaendelea kusema:

“Suala hapa sio kurahisisha uhusiano wa kibinafsi kati ya mawaziri hao wawili wa mambo ya nchi za nje wa eneo ,bali cha muhimu hapa ni kuhimiza ushirikiano kati ya serikali za nchi hizi mbili nkatika mada muhimu.”

Bila ya ushirikiano pamoja na Pakistan,juhudi za kuleta utulivu nchini Afghanistan haziwezi kufanikiwa-anasema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier.

Hali nchini Afghanistan si tulivu hivyo,kinyume na vile wanavyopendelea iwe viongozi wa mataifa tajiri kwa viwanda.Wengi wao wametuma wanajeshi nchini Afghanistan..Siku chache tuu zilizopita wanajeshi watatu wa jeshi la shirikisho Bundeswehr wameuliwa kufuatia shambulio la kujitolea mhanga maisha huko Kunduz.Serikali ya Pakistan inahoji ushawishi wake kwa wataliban unakikomo.Serikali ya mjini Kabul lakini inahisi hizo ni mbinu tuu za kutaka kujitoa.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Afghanistan Rangin Dadfar Spanta atakaehudhuria mkutano wa G8 mjini Postdam aliiambia hivi karibuni Deutasche-Welle,tunanukuu:

“Tuonavyo sisi ni kwamba yote haya yanaungwa mkono na serikali.Na hasa idara ya upelelezi ya Pakistan na baadhi ya wanajeshi wanahusika.”Mwisho wa kumnukuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Afghanistan.

Inadhaniwa kwamba mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa G8 watawatanabahisha na kuwasihi wenzao wa Afghanistan na Pakistan juu ya umuhimu wa kulindwa mipaka ya nchi hizo mbili.

Mbali na mada hiyo,mvutano uliosababishwa na mradi wa kinuklea wa Iran nao pia utajadiliwa wakati wa mkutano wa mambo ya nchi za nje wa mataifa tajiri kwa viwanda G8 mjini Postdam.Baada ya ripoti ya hivi karibuni ya shirika la kimataifa la nguvu za atomiki kuzungumzia juu ya Iran kuendelea na mipango yake ya kurutubisha maadini ya uranium,Marekani imetoa mwito vikwazo vizidishwe dhidi ya serikali ya Teheran.Marekani inaitaka pia serikali ya Iran iache kuwapatia misaada ya fedha na silaha wanamgambo wa kishiya nchini Irak.Kwa upande wake serikali ya Iran inahoji kwamba wanajeshi wa Marekani ndio sababu ya kuzidi matumizi ya nguvu nchini Irak.Jumatatu iliyopita,wanadiplomasia wa Iran na Marekani walikutana kwa mara ya kwanza kwa mazungumzo mjini Baghadad baada ya kupita zaidi ya miaka 25.

Mzozo kuhusu mustakbal wa jimbo la kusini mwa Serbia-Kosovo,utajadiliwa pia na mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa tajiri kwa viwanda G-8 watakaokutana katika kasri la Cecilienhof mjini Postdam.Mkutano huo umelengwa kuandaa mkutano wa kilele wa viongozi utakaoitishwa wiki ijayo mjini Heiligendamm.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com