Mkutano wa Kimataifa wa uchumi waendelea Cape Town | Masuala ya Jamii | DW | 06.05.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Mkutano wa Kimataifa wa uchumi waendelea Cape Town

Wajumbe kwenye mkutano wa Cape Town wamesema uchumi wa nchi za Kiafrika ni miongoni wa chumi zinazokua kwa kasi, lakini haujaboresha hali ya maisha.

default

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma

Rais Jacob Zuma amesema bara la Afrika linahitaji kuanzisha mahusiano mapya duniani yatakayoipa bara hilo nafasi kubwa zaidi ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya Uchumi wa dunia. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi wa 21 mjini Cape Town, Afrika Kusini jana, rais Jacob Zuma amesema mahusiano yaliyopo baina ya eneo la Kaskazini na Kusini la dunia ni tofauti.

Rais Jacob Zuma amesema bara la Afrika lisiwe tena bara la kuzalisha mali ghafi na kuziuza nje pekee. Zuma ambaye amekuwa mstari wa mbele kushinikiza nchi zinazoendelea kushirikishwa kikamilifu katika taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa na Taasisi ya Fedha Dunia, amasema nchi zinazoinukia kiuchumi zinastahili sifa kwa kuzuia msukosuko wa uchumi duniani uliotokea mwaka 2008.

Mapema wataalamu walihimiza Afrika kuongeza mahusiano na masoko ya dunia ili kuongeza ushindani, na kuweza kuhimili ukuaji mkubwa wa uchumi unaotarajiwa mwaka huu. Jennifer Blake, Mkuu wa kituo cha ushindani cha Uchumi wa Dunia, amesema, Uchumi wa nchi za Afrika uliweza kuhimili dhoruba ya msukosuko wa uchumi duniani uliotokea mwaka 2008, na kutikisa nchi zilizoendelea duniani.

Tangu kipindi hicho Uchumi wa nchi za Afrika umeanza tena kukua ukionyesha hali nzuri ambayo kwa bahati mbaya hata hivyo haukuweza kuonyesha nguvu yake katika masoko ya dunia.

Jennifer Blake anasema hii inaonyesha dhahiri kuwa Uchumi wa Barani Afrika haujajumuishwa kikamilifu kwenye masoko ya dunia. Mkuu huyo wa kituo cha ushindani cha Uchumi wa Dunia, amesema japokuwa hali hii inazikinga nchi barani Afrika, kutokana na misukosuko kama hiyo, lakini hii itakuwa kikwazo katika maendeleo ya uchumi hapo baadaye.

Taasisi ya Fedha Duniani imetabiri kuwa uchumi wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara utakuwa kwa asilimia 5.5 mwaka huu, mmoja ya ukuaji mkubwa duniani, lakini wameonya kuwa endapo uchumi wa dunia utatetereka kidogo, bara la Afrika litaumia. Shantayanan Devarajan, Mchumi mkuu wa Benki ya Dunia, Afrika, amesema ushindani ndio utakaoleta tofauti, hata kama uchumi wa Afrika utahimili au la.

Shirika la ushauri la Ernst $ Young lilisema siku ya Jumanne kuwa uwekezaji wa nje barani Afrika umekuwa kwa asillimia 87 katika muongo uliyopita, kwa sababu ya kuonyesha ukuaji ulio imara na faida za juu. Shirika hilo limesema uwekezaji wa moja kwa moja ulipanda kwa kasi kutoka miradi mipya 338 barani Afrika mwaka 2003 hadi kufikia 633 mwaka jana.

Nchi kumi za barani Afrika zilizovutia asilimia 70 ya uwekezaji huo ni pamoja na Afrika Kusini, Misri, Morocco, Algeria, Tunisia, Nigeria, Angola, Kenya, Libya na Ghana. Shirika hilo limesema uwekezaji katika miradi mipya unatarajiwa kuanzia mwaka ujao unaokadiriwa kufikia Euro bilioni 150 hadi mwaka 2015.

Mkutano huo wa Jukwaa la Uchumi duniani unaohudhuriwa na zaidi ya wajumbe 900, unatarajiwa pia kuzungumzia suala la jinsi nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zinaweza kuendeleza ukuaji na kuongeza uwezo wake kichumi.

Mwandishi: Rose Athumani/ AFP

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 06.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11ATH
 • Tarehe 06.05.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11ATH

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com