1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mkutano wa jumuiya ya ASEAN kuanza Ijumaa

Josephat Charo
9 Novemba 2022

Uhasama kati ya Marekani na China na majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini ni masuala yatakayougubika mkutano wa nchi za kusini mashariki mwa Asia utakaohudhuriwa na rais wa Marekani Joe Biden.

https://p.dw.com/p/4JFW9
Indonesien | ASEAN Dringlichkeitssitzung zu Myanmar
Picha: Galih Pradipta/AP Photo/picture alliance

Viongozi kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya nchi za kusini mashariki mwa Asia ASEAN watakutana mjini Phonm Penh kuanzia Ijumaa, kuanzisha mchakato wa kidiplomasia katika eneo hilo ambao pia utaujumuisha mkutano wa nchi tajiri na zinazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani za G20 huko Bali Indonesia na mkutano wa kilele wa jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi wa Asia na Pasifiki, APEC huko Bangkok.

Utawala wa rais Biden umeitambua China kama mshindani na hasimu mkubwa wa Marekani ukisema utawala wa mjini Beijing unajaribu kuubadili muundo wa kiutawala wa dunia kuendana na mfumo wake wa utawala wa kiimla.

Akifanya ziara yake ya pili barani Aeia mwaka huu chini ya kiwingu cha uchaguzi wa kati wa Marekani, rais Biden anakabiliwa na kibarua kipevu cha kuwashawishi viongozi wa jumuiya ya ASEAN, wengi wao wakiwa wamechoka kuegema upande mmoja kati ya jirani yao mwenye nguvu kubwa, China, na mshirika wao muhimu wa kibiashara, Marekani.

Afisa wa cheo cha juu wa Marekani amesema Biden atasisitiza juu ya umuhimu wa amani katika ukanda huo, ikiwamo suala la Taiwan na kuheshimiwa kwa mfumo wa utawala wa dunia uliojikita katika msingi wa sheria.

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya ya ASEAN mwezi Agosti uligubikwa na ziara ya spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi huko Taiwan na kauli kali iliyotolewa na utawala wa mjini Beijing kujibu ziara hiyo, huku ikidai kisiwa hicho chenye utawala wake wa ndani ni sehemu ya himaya yake.

China yapania kuimarisha mahusiano na nchi za ASEAN

Waziri Mkuu wa China Le Keqiang alimpiku Biden jana Jumanne katika mbio za kufanya diplomasia alipowasili Phnom Penh kwa mazungumzo na kiongozi wa Cambodia Hun Sen.

USA | Präsident Joe Biden
Rais Joe Biden wa MarekaniPicha: Anna Moneymaker/Getty Images

Mahusiano kati ya Marekani na China yanaendelea kuvurugika kutokana na masuala mbalimbali ukiwamo mgororo kuhusu kisiwa cha Taiwan na madai ya ukiukwaji wa haki za biandami huko Xinjiang, na serikali nyingine za nchi za Magharibi zimelalamika kuhusu shughuli za China katika himaya zao pamoja na unyanyasaji na ukandamizaji wa wapinzani.

Rais wa China Xi Jinping amesema serikali ya mjini Beijing na Marekani sharti zitafute njia za kufikia maelewano na kushirikiana, lakini wakati huo huo ameendelea kutekeleza sera kandamizi ya kigeni ambayo haionyeshi heshima yoyote kwa Marekani.

Xi anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kundi la nchi tajiri na zile zinazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani za G20 huko Bali, Indonesia. Xi atakutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza na rais Joe Biden kandoni mwa mkutano huo.

Vita vinavyoendelea nchini Ukraine vinatarajiwa kuwashughulisha viongozi watakohudhuria mkutano wa jumuiya ya ASEAN. Ukraine itasaini mkataba wa ushirikiano na jumuiya ya ASEAN kesho Alhamisi, katika hatua ya kwanza kuelekea kuanzisha mahusino rasmi na jumuiya hiyo.

Viongozi pia wanatarajiwa kujadili hali ya wasiwasi inayoendelea kuongezeka katika eneo la Korea, ambako Korea Kaskazini ilifanya majaribio kadhaa ya makombora wiki iliyopita.

(afp)