1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Istanbul kuhusu Irak

Oummilkheir2 Novemba 2007

Mvutano kati ya Uturuki na waasi wa kikurd wa PKK unatishia mazungumzo ya nchi zinazopakana na Irak mjini Istanbul

https://p.dw.com/p/C7fa
Helikopta ya Uturuki karibu na eneo la kaskazini mwa Irak
Helikopta ya Uturuki karibu na eneo la kaskazini mwa IrakPicha: picture-alliance/ dpa

Wanasiasa wa kutoka nchi 17 na wawakilishi wa mashirika kadhaa ya kimataifa wamekutana mjini Istanbul nchini Uturuki hii leo kuzungumzia hali namna ilivyo nchini Irak.

Katika mkutano huu wa pili wa aina yake,wa kwanza uliitishwa mwezi May nchini Misri,wajumbe walikua wazungumzie hasa hali namna ilivyo nchini Irak.Lakini kitisho cha Uturuki cha kulivamia eneo la kaskazini la Irak kuwaandamana waasi wa kikurd wa chama cha PKK,kimegubika mazungumzo ya mjini Istanbul.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amepangiwa kukutana kwanza na rais Abdallah Gül kabla ya kuhudhuria mkutano huo pamoja na wawakilishi wa umoja wa ulaya,jumuia ya mataifa tajiri kiviwanda G8 na jumuia ya nchi za kiarabu.

Irak inahofia maendeleo yaliyoweza kupatikana katika juhudi za kuimarisha usalama hazitatajwa wakati wa mkutano huo wa Istanbul.Waziri wa mambo ya nchi za nje Hoschjar Sebari alionya mapema mkutano wa Istanbul usije ukagubikwa na mzozo kati ya Uturuki na waasi wa PKK.

Serikali ya mjini Baghdad iliyowakilishwa mjini Istanbul na waziri mkuu Nouri el Maliki ilitaka kuzungumzia ufanisi uliopatikana katika kuimarisha usalama nchini Irak.Walitaka pia lizungumziwe tatizo la kupatiwa watu nishati nchini Irak na hatima ya wakimbizi milioni nne walioyapa kisogo maskani yao,tangu wale walioko ndani na wengineo waliokimbilia nje ya Irak.

Uturuki ,mwenyeji wa mkutano huo inataka pia papatikane ridhaa miongoni mwa washiriki.Waziri wa mambo ya nchi za nje Ali Babacan amesisitiza nchi yake haitoshinikiza pekee mzozo wake pamoja na PKK ujadiliwe.Lengo la serikali ya Ankara amesema waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki ni kuhakikisha umoja na utulivu wa Irak ili kuepukana na kitisho cha kuzuka mtafaruku katika eneo lote hilo.

Pembezoni mwa mkutano huo,waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyeb Erdogan alizungumza na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Cindoleezza Rice aliyewasili Ankara leo ili kuwatanabahisha viongozi wa nchi hiyo shirika waachane na hatua za kulivamia eneo la kaskazini la Irak kuwaandama waasi wa PKK.

Mwishoni mwa mazungumzo yao,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alisema.

“”Sote tunabidi tuzidishe mara dufu juhudi zetu na Marekani imeahidi kufanya hivyo hivyo.Tunabidi kulishughulikia kwa makini tatizo hili.Nitarudia tena si rahisi kuwandama magaidi waliojificha katika maeneo ya mbali kama hivyo hivyo-ni tatizo kubwa.”

Waziri Condoleezza Rice alizungumza pia na rais Abdullag Gül na waziri mwenzake wa Uturuki Ali Babacan.

Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani imelengwa kuandaa mazungumzo ya jumatatu ijayo mjini Washington kati ya waziri mkuu wa Uturuki Edogan na rais George W. Bush.

Waziri Condoleezza Rice atakwenda Istanbul baadae hii leo kwa mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa Irak Nouri el Maliki.Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anataka papatikane msimamo wa pamoja wa washirika wote wawili wa Marekani-Irak na Uturuki kuelekea mzozo wa PKK.Anataka kushauri,wamarekani,waturuki na wairak ,kwa pamoja waandame waasi wa PKK.

Kesho waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani atahudhuria mkutano wa mawaziri kuhusu Irak,mkutano unaohudhuriwa pia na madola makuu.

Maandamano yanafanyika mijini Ankara na Instanbul wakati wa ziara ya waziri Condoleezza Rice kulaani PKK.