1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G20 waendelea leo

Kabogo Grace Patricia12 Novemba 2010

Mkutano huo unahudhuriwa na viongozi wa mataifa tajiri duniani na yale yanayoinukia kiuchumi ya G20.

https://p.dw.com/p/Q6df
Rais Barack Obama wa Marekani na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria mkutano wa G20, Korea Kusini.Picha: AP

Mkutano wa kilele wa mataifa tajiri duniani na yale yanayoinukia kiuchumi ya G20, unaendelea hii leo katika mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul. Mkutano huo wa siku mbili unaohudhuriwa na viongozi wa mataifa ya G20, una lengo la kuangalia uwiano ambao hauko sawa wa kibiashara duniani, madai ya kupunguza thamani ya fedha pamoja na njia za kutuliza masoko ya fedha duniani.

Mapema, uamuzi uliotolewa na viongozi wa G20 wa kutotekeleza pendekezo la Marekani la kuyataka mataifa yanayosafirisha bidhaa kwa wingi nje kama vile Ujerumani yadhibiti kiwango cha mapato ya ziada ya biashara, ulionekana kama ushindi kwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Viongozi wa G20 wanatarajiwa kupitisha masharti mapya ya benki na makali, pamoja na kulifanyia mageuzi ya Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, hatua itakayofungua njia kwa mataifa yanayoinukia na yale yanayoendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika chombo hicho cha Umoja wa Mataifa. Mkutano huo wa kilele wa G20 unamalizika hii leo.