1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G-7,Kanada

5 Februari 2010

Vipi kuseleleza kustawi uchumi ?

https://p.dw.com/p/LtR1
Rainer Bruederle-waziri wa uchumi.Picha: AP

Mawaziri wa fedha wa kundi la nchi 7 - tajiri kabisa ulimwenguni,G-7 pamoja na marais wao wa Banki kuu , wamewasili leo mjini IQALUIT, kaskazini kabisa mwa Kanada ,kwa kikao chao cha siku 2 chenye shabaha ya kutilia nguvu juhudi za kuufufua uchumi ulimwenguni kufuatia msukosuko wa fedha duniani.Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Tume ya Umoja wa Ulaya,zinahudhuria pia kikao hiki cha G-7.

Wajumbe katika kikao hiki cha siku 2 huko Kanada,wanaotoka Marekani,Ujerumani,Ufaransa,Itali,Japan na Uingereza, waliombwa kabla ya kuwasili ,kuacha suti na tai zao nyumbani na kuvaa tu masueta ya joto wakiwa huko Iqaluit, mji uliopo kiasi cha Km 2000 kaskazini mwa Montreal.

Kikao hiki hakipangi kutoa taarifa ya mwisho ya mkutano itakayochambua fikra au hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali zao .Badala yake, mawaziri hao wa fedha, wataitisha mkutano na waandishi habari kesho Ijumamosi, ambamo waziri wa fedha wa Kanada Jim Flaherty,ataeleza ingawa kwa muhutasari tu, kile kilichozungumwa faraghani na wajumbe wa kundi hilo la G-7.

Mazungumzo yatazamiwa kutuwama juu ya hali za sasa za kiuchumi za kundi hilo la G-7 kwa lengo la kuimarisha hali ya sasa ya kurejea kustawi kwa uchumi pamoja na marekebisho ya sheria ya kudhibiti masoko ya fedha ili kuzuwia hatari zilizochochea kuporomoka kwa mabenki .Jinsi ya kuongoza mfumo wa fedha, litabakia swali la kuzungumzwa.

Ujerumani,Ufaransa na Itali , zinatazamiwa katika kikao hiki, kurejea upya mwito wao wa kutungwa sheria za kimataifa kuzima mchezo wa kamari katika masoko ya fedha nje ya mipaka yao.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Rainer Bruderle,alisema jana kuwa hakuna taifa pekee linaloweza pekee yake kufanya mageuzi ya masoko ya fedha.

Afisa wa hadhi ya juu wa wizara ya fedha ya Marekani, amesema nae kuwa sarafu ya China (Yuan) ambayo thamani yake iko chini kuliko inavyostahiki,itakuwa pia mada ya kuzungumzwa katika kikao hiki.Mvutano tangu wa kibiashara hata wa kisiasa, umeibuka hivi punde kati ya China na Marekani. Kikao hiki cha G-7 kinamalizika kesho.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman