1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa dharura wa FAO, Roma

26 Julai 2011

Umoja wa mataifa umetaka pachukuliwe hatua kubwa ya kivitendo, kukabiliana na janga la njaa katika pembe ya Afrika wakati kesho 27.07.11 kutafanyika mkutano wa nchi fadhili mjini Nairobi -Kenya

https://p.dw.com/p/123On
Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa mataifa, FAO, limejadili hali ya njaa na ukame katika pembe ya AfrikaPicha: picture alliance/dpa

Mkuu wa shirika hilo la chakula na kilimo la Umoja wa mataifa Jacques Diouf amesema hali mbaya ya ukame na njaa katika pembe ya Afrika inahitaji msaada mkubwa na wa dharura wa jamii ya kimataifa. Lakini wakati Diouf akieleza hayo, jumuiya za misaada zimeshutumu kile kilichotajwa kuwa ni ahadi ndogo zilizotolewa hadi sasa .

Diouf / FAO / Welternährungsgipfel / Rom
Jacques Diouf, Mkuu wa FAOPicha: AP

Maafisa wamesema umoja wa mataifa umepokea kiasi ya dola bilioni moja, tangu ulipotoa wito wa kwanza wa msaada kwa ajili ya Kanda hiyo ya pembe ya Afrika Novemba mwaka jana, lakini unahitaji dola bilioni moja zaidi ifikapo mwisho wa mwaka huu kukabiliana na hali ya dharura.

Benki ya dunia imeahidi kutoa dola milioni 500 zaidi, huku sehemu kubwa ya fedha hizo ikikusudiwa miradi ya muda mrefu ya kuwasaidia wafugaji, wakati dola milioni 12 zitakua ni kwa matumizi ya msaada wa haraka kwa waliokumbwa na janga hilo la ukame na njaa.

Inakadiriwa watu wapatao milioni 3.7 nchini Somalia, ikiwa ni theluthi moja ya idadi ya wakaazi wa nchi hiyo wanakabiliwa na kitisho kikubwa cha njaa na mamilioni wengine nchini Djibouti, Kenya, Ethiopia na Uganda wamekumbwa na ukame mbaya kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 60 iliopita.

Rom UN-Treffen zur Hungersnot in Afrika
Picha: picture alliance/dpa

Lakini jumuiya za misaada zimeelezea kuvunjwa moyo mno na hatua za jamii ya kimataifa. Barbara Stocking ambaye ni mkuu wa Shirika la misaada la Uingereaza OXFAM amesema ni aibu kuwa ni nchi chache tu tajiri na zenye uchumi wenye nguvu zilizoonyesha nia ya kusaidia leo hii, kuyanusuru maisha ya wengi miongoni mwa walio masikini. Msanii wa kundi la muziki la U´2 na mwanaharakati anayepigana dhidi ya umasikini BONO, amesema nia ya kisiasa ilioonyeshwa mjini Roma katika mkutano wa jana sasa haina budi ifuatiwe na vitendo.

Switzerland World Economic Forum Davos Bono
Muimbaji mashuhuri, BonoPicha: AP

Waziri wa kilimo wa Ufaransa, Bruno Le Maire akasema ikiwa hatua zinazohitajika hazitachukuliwa , janga la njaa litageuka kuwa kashfa ya karne. Hata hivyo akihutubia mkutano huo wa Roma, Mkuu wa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa WFP, Josette Sheeran aliahidi kujitolea kwa shirika hilo kuchukua hatua.

Macho na masikio sasa yanaelekezwa Nairobi ambapo kesho, Umoja wa mataifa umeandaa mkutano wa wafadhili, kuchangisha fedha za kuwasaidia waathirika wa janga hilo la ukame na njaa katika pembe ya Afrika.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman /afp
Mhariri: Yusuf, Saumu