1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Berlin 2009

29 Aprili 2009

Mada kuu ya mkutano unaofanywa katika Chuo Kikuu cha Humboldt katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin ni ugawaji wa ardhi na matumizi yake.Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa serikali wa zamani kutoka bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/HggI
Rais wa zamani wa Ghana,Jerry Rawlings.Picha: AP

Chuo Kikuu cha Boston kiliwaalika Berlin takriban viongozi 12 wa zamani kutoka Afrika.Miongoni mwao ni wapenda mageuzi kama vile Festus Mogae kutoka Botswana,John Kufuor kutoka Ghana na Aristides Pereira kutoka Cape Verde.Majadiliano yaliyofanywa bila ya kuwepo waandishi wa habari hasa yalihusika na mada ya kisiasa:yaani mageuzi ya sera za ardhi pamoja na matumizi na ugawaji wa ardhi barani Afrika.

Rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings aliekuwa madarakani hadi mwaka 2001 baada ya kushika wadhifa huo kufuatia mapinduzi ya mwaka 1981 amesema:

"Tangu miaka na miaka,suala la matumizi ya ardhi na ugawaji wa ardhi hiyo limesababisha migogoro mingi.Mara kwa mara masuala yanayohusika na ardhi yameamuliwa na serikali kisiasa na kisheria.Hali hiyo imesababisha uhasama miongoni mwa umma na machifu wa kimila."

Rawlings amealikwa Berlin na Charles R.Stith ambae hiyo miaka minane iliyopita alianzisha duru ya majadiliano miongoni mwa marais wa zamani. Stith aliekuwa balozi wa Marekani nchini Tanzania kwa miaka kadhaa alitaka kuwapa wanasiasa wapenda mageuzi kutoka Afrika fursa ya kukutana na kujadiliana.Kwa maoni yake demokrasia ni mtindo unaozidi kuenea barani Afrika na wale wanaopigania mageuzi hayo wanapaswa kusaidiwa na kupewa jukwaa la kubadilishana maoni.

Kituo cha utafiti kuhusu bara la Afrika kilichoanzishwa na Stith katika Chuo Kikuu cha Boston hakishughulikii midahalo ya kinadharia. Zaidi hushughulikia siasa zinazotoa umuhimu kwa Afrika iliyojikomboa na inayoanzisha mfano wake wenyewe na ikitafuta jawabu kwa masuala yanayohusika na Afrika.Na viongozi hao wa zamani ni muhimu, kwani wao wanaelewa changamoto za kisiasa, masharti ya uongozi wa kisiasa nchini mwao na barani Afrika kwa jumla.Kwa hivyo itakuwa hasara ikiwa viongozi hao wanapoondoka madarakani hawatoshauriwa au shirikishwa katika majadiliano yanayohusika na masuala ya mustakabali wa bara la Afrika.

Mkutano wa mwaka 2009 umefanywa mjini Berlin kule kule ambako miaka 125 iliyopita wakoloni waliitisha mkutano wa kuligawa bara la Afrika na kuchora mipaka bila ya kuwaauliza Waafrika maoni yao.

Mwandishi: U.Schaeffer/P.Martin

Mhariri: Abdul-Rahman