1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa amani Mashariki ya Kati kufanyika Marekani

21 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CPlu

Marekani itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa Mashariki ya Kati hapo tarehe 27 mwezi wa Novemba wenye lengo la kufufuwa mchakato wa amani ulio mahtututi.

Mbali na Israel na Wapalestina Marekani imezialika nchi kadhaa zikiwemo nchi muhimu za Kiarabu Saudi Arabia na Syria katika mkutano huo utakaofanyika Annapolis,Maryland. Mkutano huo pia utahudhuriwa na kamati ya ufuatiliaji ya Umoja wa Waarabu,nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, nchi wanachama wa Kundi la Mataifa Manane yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani G8 na wahusika wengine wakuu wa kimataifa.

Rais George W. Bush wa Marekani atahudhuria mkutano huo na baadae atakuwa na mkutano mwengine na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas katika Ikulu ya Marekani.

Marekani inataraji mkutano huo utazinduwa mazungumzo rasmi ya kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

Wiki moja kabla ya kufanyika kwa mkutano huo viongozi wa Misri na Israel wana imani kwamba makubaliano ya amani yanaweza kufikiwa hapo mwaka 2008.

Akizungumza mjini Cairo kufuatia mkutano wake na Rais Hosni Mubarak wa Misri Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema kwamba mkutano huo utashughulikia masuala yote ya mzozo wa Israel na Wapalestina.