Seneta Hillary Clinton amwuunga mkono Obama.
27 Agosti 2008Seneta wa jimbo la New York Hillary Clinton ametoa mwito kwa wafuasi wake wote wamwuunge mkono seneta Barack Obama anaegombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Demokratik.
Seneta Clinton ametoa mwito huo katika siku ya pili ya mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika mjini Denver, Colorado.
Seneta Clinton amewataka wafuasi wake wasimame pamoja ili wamwezeshe Barack Obama kuingia Ikulu ya Marekani kama rais.
Hillary Clinton alieshindwa na Obama katika kugombea nafasi ya kukiwakilisha chama cha demokratik ,amesema sasa wakati umefika kwa wote kusimama kama chama kimoja. Aliwaambia wajumbe zaidi ya alfu nne wanaohudhuria mkutano mkuu wa chama hicho, kuwa Obama ni mjumbe wake na lazima awe rais . Huku akishangiliwa kwa mayowe ya furaha , seneta huyo wa jimbo la New York aliendelea kusema asilani ,abadan, hakuna cha MacCain.
Amesema hakutumia miaka 35 iliyopita katika mahandaki kutetea haki za watoto, kuendesha kampeni ili wamarekani wote wapate huduma za afya, na wala hakutumia miaka hiyo kuwasaidia wazazi, familia, na kutetea haki za akina mama nchini Marekani na duniani kote, halafu kuja kumwona mtu mwengine wa chama cha Republican akiingia katika Ikulu. "Hapana"
Amewataka wamerekani wote milioni 18 waliompigia kura katika uchaguzi wa kutafuta mjumbe wa kukiwakilisha chama cha demokratik kugombea urais, sasa wasimame pamoja na Obama.
Amesema wote sasa wamo katika timu moja, na hakuna anaeweza kusimama kando katika mapambano ya kutetea mustakabal wa Marekani.
Ametamka kuwa lazima chama cha demokratik kishinde katika mapambano hayo.
Akiwahutubia wajumbe kwenye mkutano huo aliekuwa gavana wa jimbo la Virginia Mark Warner amesema kuwa seneta Obama ndiye mtu atakeifaa Marekani. Amesema uchaguzi wa rais nchini Marekani safari hii ni mashindano ya kupigania mustakabal wa nchi.
Gavana huyo wa zamani ameeleza kuwa Marekani haitaweza kuzikabili changamoto za ushindani za karne ya 21 ikiwa itaongozwa na rais alienaswa katika zama zilizopita.
Gavana huyo wa zamani Warner pia ameulaumu utawala wa rais Bush kwa kutumia sera potovu na itikadi za kizamani katika uongozi wake.
Wajumbe kwenye mkutano mkuu wa siku nne wa chama cha demokratik wanatarajiwa kumpitisha rasmi seneta Barack Obama kugombea urais wa Marekani mnamo mwezi novemba.