1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu Afrika mjini Accra

Josephat Charo2 Julai 2007

Uwezekano wa kuunda nchi moja ya Afrika unatathminiwa kwenye mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Afrika mjini Accra, Ghana. Viongozi wa serikali na viongozi wa nchi kutoka sehemu mbalimbali za bara hilo walianza mkutano wao wa siku tatu hapo jana Jumapili utakaomalizika kesho Jumanne. Kati ya wanachama 53, 30 wanawakilishwa na viongozi wao.

https://p.dw.com/p/CB37
Alpha Oumar Konare
Alpha Oumar KonarePicha: AP

Mada mbiu katika ajenda ya mkutano wa mjini A ccra Ghana ni utawala wa bara la Afrika. Ripoti ya uchunguzi uliofanywa mwaka jana na Umoja wa Afrika iliyopewa jina, An African Union Government: Towards the United states of Africa, imependekeza kwamba utawala wa aina hiyo unaweza kuanza kufanya kazi kufikia mwaka wa 2015, hivyo kukamilisha nia ya umoja wa zamani wa Afrika, OAU.

Huku baadhi ya viongozi wakisita kuhusu kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Afrika, wengine wanaamini ni muhimu kuisaidia kujikwamua kutokana na umaskini na maendeleo duni. Mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika, Alpha Oumar Konare, alisema ipo haja ya kukabiliana na ukweli na kuunda nchi moja ya Afrika.

Aidha kiongozi huyo alisema muungano wa kisiasa utalipa bara la Afrika ushawishi mkubwa wakati linapojadiliana na maeneo mengine duniani. Konare alisema Afrika ina bunge na mahakama ya katiba lakini vyombo hivi havina mamlaka na utendaji wake ni duni. Serikali ya umoja wa Afrika itavipa vyombo hivi mamlaka ya kufanya kazi.

Bunge la Afrika liliundwa mnamo mwaka wa 2004 lengo mojawapo likiwa ni kuendeleza utawala bora na demokrasia barani Afrika. Huku sheria ya kuunda mahakama hiyo ikiwepo, inaweza kuanza kutekelezwa wakati itakapoidhinishwa na wanachama wote wa Umoja wa Afrika. Kufikia sasa ni wanachama wachache tu walioidhinisha sheria hiyo.

Rais wa Libya, Muamar Gaddafi, hakuwepo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mjini Accra Ghana. Rais wa Ghana, John Kufuor, alisisitiza ni muhimu kukusanya maoni ya Waafrika wenyewe kuhusu serikali ya Umoja wa Afrika na pia makundi ya kanda mbalimbali barani Afrika yanahitajika kuunda serikali hiyo.

Ukosefu wa usafiri huru wa watu na bidhaa katika maeneo mbalimbali inasemekana umepunguza maingiliano. Takwimu kutoka kwa tume ya uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika, zinaonyesha uchumi katika kamati ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi ni asilimia 25 ya biashara ya eneo hilo na Ulaya. Mwito wa kutaka watu watembee huu ulitolewa na watetezi waliohudhuria mkutano wa mjini Accra.

´Tunawatolea mwito waheshimiwa waondoe mahitaji ya visa za kusafiria kwa Waafrika waweze kusafiri kila nchini kama sehemu ya kwanza kufikia sheria ya kibali cha kuishi, kufanya kazi na kutembea. Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na makundi 150 ya kijamii kutoka nchi 30 za kiafrika, watetezi walisema bila uraia wa bara zima, serikali ya Umoja wa Afrika haina maana.´

Watetezi pia wamechukua msimamo kuhusu mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi, inayotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka ujao, na ambayo wengi wanaamini itazitumbukiza nchi nyingi barani Afrika katika umasikini zaidi. Mamia ya watetezi waliovalia fulana zenye ujumbe wa kupinga mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi, ´Say No to EPAs´ waliandamana nje ya eneo la mkutano wa mjini Accra mwishoni mwa juma lililopita.