1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuadhimisha miaka 20 ya Itifaki ya Montreal

P.Martin17 Septemba 2007

Wajumbe wa nchi 190 hii leo wanakutana Montreal,Kanada kujadiliana njia za kupambana na ongezeko la ujoto duniani na kurekebisha tabaka la hewa ya ozoni.

https://p.dw.com/p/CB1B

Majadiliano yanayoanza leo Jumatatu ni sehemu ya mkutano uliodhaminiwa na Umoja wa Mataifa kuadhimisha miaka 20 tangu kutiwa saini Itifaki ya Montreal.Huo ni mkataba wa kimataifa wenye lengo la kukomesha uzalishaji wa michanganyiko ya kemikali ambazo hupunguza tabaka la hewa ya ozoni.

Nchi zilizotia saini Itifaki ya Montreal na ambazo hupunguza uzalishaji wa kemikali zinazodhuru tabaka la hewa ya ozoni,zinatumaini kupata njia ya kuondoa gesi za HCFC ambazo zimetoboa tabaka la hewa ya ozoni katika eneo la Antaktiki.

Umoja wa Mataifa unasema,kusawazishwa kwa tabaka hilo,kutasaidia pia kupambana na ongezeko la ujoto duniani,ambao katika miaka ijayo huweza kusababisha madhara makubwa mno kwa hali ya hewa,vima vya bahari,wanyama na mimea.

Kwa mujibu wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaepigia debe juhudi za kupunguza ongezeko la joto duniani,mataifa yanayochafua mazingira yanapaswa kuchukua hatua za kuhifadhi mazingira yetu.

Kwa maoni ya Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan,Itifaki ya Montreal iliyotiwa saini mwaka 1987 imeleta mafanikio zaidi,kuliko jitahada zingine zote za kimataifa,kupambana na tatizo la dunia.

Ni matumaini ya wagombea mazingira kuwa majadiliano ya Montreal yatazaa matunda kama Itifaki ya Kyoto ya mwaka 1997,kuzuia uzalishaji wa gesi zinazokusanyika hewani.Gesi hizo zinaruhusu miale ya jua kujipenyeza,lakini joto linalokusanyika hewani,halina njia ya kutoweka.

Ingawa Itifaki ya Kyoto imeweka viwango kuhusu gesi zinazochafua mazingira,nchi kama Kanada, Marekani na India hazitekelezi matakwa hayo.China imetia saini makubaliano hayo,lakini kwa hivi sasa,inasamehewa kwa sababu ya kuhesabika kama nchi inayoendelea.

Tangu kuanzishwa kwa viwanda duniani na viwango vya gesi kutoka viwanda hivyo kuzidi kuongezeka, ujoto duniani umezidi kwa kiwango kinachotisha.Ongezeko hilo la joto pia linalaumiwa kuwa limesababisha barafu kuanza kuyayuka katika ncha za dunia.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi-Mtendaji wa Mradi wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa,bwana Achim Steiner,ongezeko la ujoto duniani,linaweza kupunguka kwa asilimia 4.5 ikiwa uzalishaji wa gesi za HCFC utaweza kuzuiliwa na kukomeshwa kabisa katika kipindi cha miaka 10 ijayo.