1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano juu ya Afghanistan The Hague.

31 Machi 2009

Iran yapinga majeshi ya kigeni Afghanistan

https://p.dw.com/p/HNTX
Clinton-waziri wa nje.Picha: AP

Wajumbe kutoka nchi 90 ulimwenguni-usoni kabisa waziri wa nje wa Marekani, Bibi Hillary Clinton, wameanza mjini The Hague,Uholanzi, mkutano unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa juu ya mustakbala wa Afghanistan.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan, anahudhuria sawa na waziri mdogo wa mambo ya nje wa Iran ambayo imeitikia mualiko wa Bibi Cliton, lakini katika taarifa yake ya hivi punde kabla kuanza mkutano, imepinga kuwapo majeshi ya kigeni nchini Afghanistan.Msimamo huu unapingana na juhudi za utawala wa Rais Barack Obama,ulioinyoshea Iran mkono wa maskizano.

Marekani inatazamia kuungwamkono na nchi hizo 90 zinazohudhuria mkutano huu , kuchangia zaidi vikosi na katika maendeleo ya kiuchumi ,kukijenga kikosi cha polisi na jeshi la Afghanistan -ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Rais Obama wa kupambana na Wataliban na Al Qaeda.

Akichambua mkakati wake huo ,Rais Obama alinadi:

"Tuna shabaha wazi kabisa-nayo ni kuchafua,kuwangoa na kuwashinda kabisa Alqaeda nchini Afghanistan na Pakistan na kuona hawarejei tena katika nchi zote mbili."

Utayarifu wa Iran kushiriki mkutano huu, kulionekana ni ishara ya mwanzo ya kunyemeleana tena baina ya Iran na Marekani ,tangu pale Rais Obama kuingia madarakani Januari 20.

Kiasi cha wanajeshi 70,000 wa Marekani na wa Shirika la Ulinzi la Magharibi (NATO) wako nchini Afghanistan wakipambana na uasi wa waumini wa madhehebu ya sunni -watalibani ambao wanaeneza itikadi kali na ushawishi wao hadi nchi jirani ya Pakistan,mpakani mwa nchi hizo mbili.

Tangu kutawazwa Rais wa Marekani,Januari 20,mwaka huu, Obama ameamrisha kupelekwa askari-jeshi 17,000 wa Marekani nchini Afghanistan ili kupambana na wimbi jipya la machafuko ya wataliban na washirika wao al Qaeda.Rais Obama amepeleka pia kikosi zaidi cha askari 4000 kusaidia kulijenga jeshi la Afghanistan.

Waziri wa nje wa Marekani Hillary Clinton, aliesema hana nia ya kuzungumza moja kwamoja na wajumbe wa Iran mjini The Hague,hatahivyo, amesema kuwa, angetaka Iran kusaidia katika ulinzi wa mpakani pamoja na kuzuwia biashara ya madawa ya kulevya nchini Afghanistan.

Iran ilikua ikishirikiana juu ya hilo baada ya vikosi vilivyo ongozwa na Marekani kuivamia Afghanistan 2001 ili kuuitimua madarakani utawala wa watalibani-alikumbusha bibi Clinton.Nae Richard Holbrooke,mjumbe maalumu wa Marekani kwa Afghanistan na Pakistan, amekumbusha kwamba kuhudhuria kwa Iran mkutanoni mjini The Hague,Uholanzi leo ni sehemu barabara ya mkakati wa kuleta amani kwa waafghani.

Waziri wa nje Bibi Clinton, ametangaza kima cha dala milioni 40 kikiwa msaada mpya wa Marekani katika mfuko wa UM wa kuandaa uchaguzi nchini Afghanistan hapo August.Na Tume ya Umoja wa Ulaya nayo, imetangaza leo itachangia dala milioni 80 kama msaada zaidi kwa Afghanistan kwa mipango ya uchanguzi huo.