Mkenya Rita Jeptoo asubiri hatma yake
16 Januari 2015Jeptoo amekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa maafisa wa kitaifa kueleza kinaga ubaga na kufichua ukweli namna alivyopata dawa hizo zilizopigwa marufuku.
Mwanachama wa tume ya matibabu ya Shirikisho la Riadha Kenya na ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji Isaac Mwangi amesema wamekusanya habari nyingi kuhusu kesi hiyo lakini bado wataendelea kushauriana. Jeptoo bado amepigwa marufuku kushiriki mashindano yoyote. Pia amesema shirikisho la riadha Kenya - AK litashauriana na Shirikisho la Riadha Ulimwenguni - IAAF kuhusu kama Jeptoo anastahili kuadhibiwa kwa kupigwa marufuku ya miaka miwili au kwa kuzingatia sheria mpya ya kupigwa marufuku ya lazima kwa miaka minne ambayo ilianza kutekelezwa Januari mosi. Kikao kingine kitaskikilizwa katika kipindi cha wiki mbili.
Meneja wa Jeptoo, Federico Rosa na kocha Claudio Berardelli, ambao wote wamejitenga na sakata hilo, pia walifika mbele ya tume hiyo. Mumewe Jeptoo, Noah Busienei -- ambaye alimshutumu Jeptoo kwa kufanya uovu huo katika mwaka wa 2011, pia alihojiwa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu