Mjerumani mwengine atekwanyara Afghanistan ? | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mjerumani mwengine atekwanyara Afghanistan ?

kuna tetzesi kwamba muandishi habari wa kijerumani anaetumikia jarida moja amenyakuliwa pamoja na mkalimani wake.

Kesi za utekaji nyara zinashughulikia katika chumba maalum ndani ya wizara ya nje ya Ujerumani

Kesi za utekaji nyara zinashughulikia katika chumba maalum ndani ya wizara ya nje ya Ujerumani

Wizara ya nje ya Ujerumani mjini Berlin, imearifu leo kwamba inachunguza taarifa kutoka Kabul, kuwa muandishi habari wa kijerumani huenda ametekwanyara nchini Afghanistan. Wiki 2 tu nyuma, wahandisi 2 wa kijerumani walinyakuliwa nchini Afghanistan na mmoja wao akafariki wakati akiwa kizuizini.

Na katika mkasa wa mahabusu 23 wa Korea ya Kusini,mtu aliedai ni msemaji wa wapiganaji wa kitaliban,amearifu leo kuwa mazungumzo ya kuachwa kwao huru yamenasa na wataliban wametishia kuanza kuwaua.

Msemaji wa wizara ya nje ya Ujerumani,Martin Jaeger amesema: “Ubalozi wetu mjini Kabul, unachunguza taarifa kuwa yamkinika muandishi habari wa kijerumani ametoweka nchini Afghanistan na tunashughulikia kufafanua haraka hatima yake.”

Nae Ajmal Khan,msemaji wa gavana wa mkoa wa Kunar,amearifu kuwa timu ya watu 3 imetumwa katika wilaya ya Watapur kuchunguza iwapo muandishi huyo wa kijerumani na mkalimani wake kweli wametekwanyara.

Kituo cha TV cha Ujerumani NTV kimeripoti kuwa maafisa wa Afghanistan wamethibitisha kutekwa nyara kwa muandishi habari wa Ujerumani asiefahamika bado ni nani huko mashariki mwa Afghanistan.

Taarifa hizi za kunyakuliwa mjerumani mwengine zimechomoza siku chache tu tangu Rüdiger Diedrich,aliekua na umri wa miaka 43 kufariki wakati akiwa kizuizini mwa watekanyara na katika hali ya kutatanisha.

Maiti yake itasafirishwa kwa ndege kuletwa Ujerumani baadae wiki hii na kuchunguzwa asili ya kifo chake-alisema msemaji wa wizara ya nje Martin Jaeger.

Kuna taarifa zisemazo muandishi huyo amekwenda katika kijiji kimoja kuchunguza ripoti kuwa raia 27 wameuwawa huklo wakati wa hujuma za anga za vikosi vya NATO.

Katika mkasa mwengine wa mahabusu nchini Afghanistan, wanamgambo wa Taliban wametishia leo kuanza kuwaua mahabusu wao 23 wa Korea ya Kusini na kufanya hivyo masaa machache yajayo ikiwa madai yao hayatatimizwa.Hii inafuatia kukwama kwa mazungumzo.

Wanamgambo wa kitaliban wametishia kuwa watawaua baadhi ya watumishi hao wa shirika la misaada la kikristu kutoka korea ya kusini iwapo wenzao 8 hawataachwa huru na serikali ya Afghanistan.

Muda wa mwisho uliowekwa na wapiganaji hao umepita-alisema Yusuf Ahmadi,msemaji wao.Ahmadi ameituhumu serikali ya Afghanistan ya rais Hamid Karzai, kuwa haioneshi uaminifu katika mazungumzo.Alisema kuwa wamewakabidhi orodha ya wafungwa 8 wa kitaliban ambao wabadilishwe na wakorea kusini,lakini serikali inapuuza-alisema.

Waasi wa kitaliban ,mabaki ya utawala wa Wataliban uliotimuliwa madarakani na majeshi yalioongozwa na Marekani 2001 kufuatia hujuma ya Septemba 11,2001 walikwisharefusha muda wao kwa masaa 24.Walikwishadai kuachwa huru wapiganaji wao 10 ili nao wamuache huru mmoja kati ya wajerumani 2 walionyakuliwa kabla.Mmoja wao ameshafariki.

Serikali ya Ujerumani inakabili msukosuko mpya wa uwezekanao wa kutekwanyara kwa muandishi habari wa kijerumani.

 • Tarehe 25.07.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHAY
 • Tarehe 25.07.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHAY

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com