1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjerumani anatunza utamaduni wa Dubai

Katharina Hagen / Maja Dreyer21 Mei 2007

Mji wa Dubai, zamani ulikuwa mji mdogo wenye bandari. Lakini katika muda mfupi umekuwa jiji kubwa. Wakitumia mapato yao ya kuuza mafuta, mashehe wa Dubai walijenga nyumba ndefu, maduka makubwa na bustani za starehe. Kinachojengwa sasa hivi ni tamthilia na jumba la sanaa. Aliyeagizwa kuandaa mbinu za kiutamaduni kwa jiji la Dubai, ni Mjerumani ambaye anatakiwa kupanda mbegu za kitamaduni katika jangwa.

https://p.dw.com/p/CHkr
Jijini Dubai
Jijini DubaiPicha: DW-TV

Mhusika wa kujenga miundo mbinu wa kiutamaduni jijini Dubai ni Michael Schindhelm, ambaye zamani aliongoza shirika la opera la jiji la Berlin. Mwanzoni mwa mwaka huu amekwenda Dubai ambapo wadhifa wake sasa ni mkurugenzi wa utamaduni.

Kwa nini ameamua kuondoka Ujerumani? Bw. Schindhelm anaeleza: “Ni jambo la pekee kabisa kwamba kuna fursa kama hiyo, yaani karatasi ni tupu kabisa na unaweza kuanza mwanzoni kabisa kujenga kituo cha utamaduni, pia katika mji ambao unaendelea haraka hivyo bila ya mfano mwingine. Kusaidia mji huo uwe pia na miundo mbino ya kiutamaduni. Au nikitumia maneno mazito zaidi ni kama kuupa mji huo roho.”

Bw. Schindhelm anataka roho ya kiutamaduni ya Dubai iwe na sura tofauti kama ndiyo sifa ya mji huo. Kwani kitu kinachofurahia Bw. Schindhelm zaidi huko Dubai ni kukutana kwa tamaduni mbali mbali: “Kuna watu kutoka kila pembe ya dunia wanaoishi hapa na kufanya kazi hapa. Yaani wanakuja hapa kuishi kwa muda. Na pia wanapeleka desturi zao kutoka nchi mbali mbali, kwa hivyo unaweza kusema kwamba mji huu utakuwa mji wa kimataifa.”

Bw. Schindhelm anatumai kituo cha utamaduni kitakuwa mahali pa kukutana, kuwasiliana na kubadilishana tamaduni tofauti. Utamaduni pia ni muhimu kwa sura ya Dubai wakati mji huo unataka kuwavutia pia watalii. Kutokana na mafuta kupungua, tayari nchi jirani zinajaribu kuwavutia watalii. Huko Abu Dhabi kumejengwa tawi la jumba maarufu la sanaa la Paris, Louvre.

Mjini Dubai pia kuna mpango wa kujenga tawi la “Disneyland”, yaani bustani kubwa la burudani. Lakini nia ya Dubai si tu kuingiza tamaduni za kutoka nje bali pia kuimarisha utamaduni wa kienyeji. Hata hivyo, kuna malalamiko kutoka Ulaya ambayo yanasema Umoja wa falme za Kiarabu hasa inanunua tamaduni za bara la Ulaya na sanii za ujenzi vile vile.

Kuhusu lawama hizo, mhusika mpya wa Dubai, Bw. Michael Schindhelm ana haya ya kusema: “Nadhani ni muhimu tusisahau kuwa barani Ulaya zamani pia hakukuwepo tamaduni za kienyeji, bali ilibidi kuzianzisha kutoka mizizi na kuzitunza vizuri ili kupatikana tamaduni na sanaa kwenye bara letu. Haya yote yametokea mamia ya miaka ya nyuma, kwa hivyo siku hizi tukifikiria tamaduni, tunadhani ni mti wenye matawi na majani mengi tu.”

Michael Schindhelm sasa ana bajeti kubwa kwa ajili ya kupanga mbegu za kiutamaduni katika ardhi hiyo ya kiarabu na kuzitunza vizuri katika miaka ijayo. Huenda katika siku za usoni, mji wa Dubai utakuwa na sura nzuri ya utamaduni kama ile ya majengo marefu ya kisasa.