1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dalili za kupatikana suluhu zaanza kuonekana

18 Desemba 2015

Wakati Marekani na mataifa mengine yenye ushawishi duniani yakijiandaa kukutana kwa lengo la kujaribu kutafuta suluhu ya mzozo wa Syria, Urusi inaonekana kuwa ndiyo yenye ufunguo wa suala hilo.

https://p.dw.com/p/1HPZz
Baadhi ya wajumbe wa baraza la usalama wa Umoja wa mataifa
Baadhi ya wajumbe wa baraza la Usalama la umoja wa mataifa.Picha: picture-alliance/dpa/J. Szenes

Ni dhahiri kuwa mataifa yatakayokuwa yakikutana hii leo mjini New York Marekani katika mazungumzo yatakayohusisha pia Umoja wa mataifa yatalazimika kujadili mpango unaoratibiwa na Urusi kwa ajili ya kipindi cha kisiasa cha mpito nchini Syria, na wenye masilahi zaidi kwa serikali iliyoko madarakani na usiokuwa na muelekeo wa kundolewa madarakani kwa Rais Bashar al Assad.

Na wakati viongozi wa mataifa hayo wakijatahidi kupata suluhu ya mzozo huo na kurejesha amani nchini humo licha ya jitihada hizo kuonekana kutozaa matunda tangu zilipoanzishwa mwaka 2011 hatua ya hivi karibuni ya Urusi kujiimarisha kijeshi na pia kushiriki katika mashambulizi ya anga nchini humo inaonekana kuipa nguvu nchi hiyo katika harakati za kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo wa Syria.

Wanadiplomasia kutoka mataifa ya Mashariki na Magharibi wanaona kuwa sasa kuna dalili za kumalizika kwa mgogoro uliopo kati ya makundi ya waasi na jeshi tiifu kwa Rais Bashar al- Assad kuliko ilivyokuwa hapo kabla.

Dola la kiisilamu lazidi kuwa tishio

Kuzidi kuongezeka kwa kitisho cha kundi la dola la kiisilamu kumechangia kuyakutanisha mataifa ambayo yamekuwa yakitofautiana kwa hoja katika masuala kadhaa na pia kuwa na misimamo inayo kinzana kukaa meza moja hivi sasa , mfano Marekani na Urusi na pia Saudi Arabia na Iran kwa madhumuni ya kuutafutia ufumbuzi wa haraka mgogoro huo wa Syria.

Maazimio hayo yanatarajiwa kupitishwa baadaye hii leo na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, yakitanguliwa na mikutano inayohusisha mawaziri wa mambo ya nchi za nje mjini New York. Baraza hilo halijawahi kupitisha maazimio ya aina hiyo katika kipindi cha nyuma.

Dalili nyingine ambazo zinaonekana kuleta matumaini kuhusiana na kutatua mzozo huo ni hatua inayoendelea sasa ya upande wa upinzani ya kuandaa wajumbe wake watakaoshiriki katika kikao cha pamoja na upande serikali kilichopangwa kufanyika mapema mwezi ujao.

Wakati hayo yakiendelea balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Samantha Power alisema mataifa hayo yenye nguvu ya kura ya veto yalikuwa bado hayajakubaliana juu ya rasimu itakayowasilishwa katika baraza hilo la usalama la umoja wa mataifa kwa ajili ya kuidhinishwa na baraza hilo baadaye hii leo.

Mataifa hayo yenye ushawishi yanaonekanakona kuwa na matumaini kuwa baraza hilo litaidhinisha mpango huo wa miaka miwili utakaohusisha mazungumzo kati ya serikali ya Syria na upande wa upinzani juu ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa na baadaye kufuatiwa na uchaguzi.

Kwa upande wake balozi wa Urusi Vitaly Churkin alisema kumekuwepo na hali ya kutokubaliana katika masuala kadhaa miongoni mwa mataifa hayo ingawa hakuwa tayari kuweka wazi masuala ambayo yanaonekana kuwa kizingiti cha kufikia makubaliano.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank -Walter Steinmeir alisema kuna hatua fulani imepigwa katika mazungumzo hayo kuhusu Syria na kusema lengo moja wapo la mkutano huo wa New York lilikuwa ni kusafisha njia katika kuandaa mazungumzo ya kutafuta amani kati ya kundi la upinzani na upande wa serikali nchini Syria.

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Urusi, Marekani, Uturuki, Saudi Arabia, Iran na mataifa mengine barani ulaya na kutoka Mashariki ya kati wanatarajia kushiriki katika mazungumzo hayo hii leo mjini New York Marekani.

Mwandishi: Isaac Gamba/ APE/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga